Naibu waziri wa ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya ameitaka bodi ya usajili wa wahandisi (ERB) Kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahandisi wote watakaokwenda kinyume na maadili ya taaluma hiyo ili kulinda maslahi ya taifa na umma kwa ujumla.
Mhandisi Kasekenya ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea ofisi ya Bodi ya usajili wa wahandisi makao makuu Jijini Dodoma kwa lengo la kuona utendaji wa taasisi hiyo,ambapo amesema kazi ya uhandisi ni muhimu sana katika kila Nyanja.
“sekta ya uhandisi hutumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo ni lazima shughuli zote zifanywe kwa kuzingatia taaluma na taratibu ili kuepusha madhara kwa wananchi. “Mradi wa uhandisi usiozingatia viwango unaweza kusababisha hasara kubwa na kuhatarisha maisha,” amesema.
Aidha Kasekenya ametoa rai kwa bodi ya usajili wa wahandisi kusimamia vema kampuni za kishauri za kihandisi ili wafanya kazi kwa weledi na kutoleta hasara kwa taifa kwa kufanya usanifu wa miradi chini ya viwango.
Pia ameitaka bodi kuweka utaratibu wa kuwachunguza wahandisi kutoka nje nchi kama wanakidhi vigezo vinavyohitajika katika usimamizi wa miradi inayotekelezwa nchini na kufanya usimamizi kwa wahandisi vijana ili wafate maadili ya taaluma hiyo.
Akisoma taarifa ya Bodi kwa niaba ya Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Bernard Kavishe, Msajili Msaidizi wa Uendelezaji wa Taaluma, Mhandisi Veronica Ninalwo, amesema ERB ina jukumu la kusimamia usajili, udhibiti na maendeleo ya taaluma ya uhandisi nchini ili kuhakikisha huduma za uhandisi zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma, maadili na usalama wa umma.
Amesema hadi Juni 2026, Bodi imesajili jumla ya wahandisi 46,084 katika ngazi mbalimbali, ambapo wahandisi wanawake ni 6,490 sawa na asilimia 14.08 ya wahandisi wote waliosajiliwa, pamoja na Mafundi Sanifu 3,762.
Aidha, Mhandisi Ninalwo amesema ERB imesajili makampuni elekezi ya kihandisi 476, yakiwemo 331 ya ndani na 145 ya nje, pamoja na maabara 56 za upimaji wa kazi na vifaa vya kihandisi.






No comments:
Post a Comment