KASEKENYA: TANROADS ISHIRIKISHE SEKTA BINAFSI KUENDESHA MAABARA ZA KISASA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 15, 2026

KASEKENYA: TANROADS ISHIRIKISHE SEKTA BINAFSI KUENDESHA MAABARA ZA KISASA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma


NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameishauri Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kushirikiana na sekta binafsi na taasisi za elimu ya uhandisi katika kuendesha maabara zake za kisasa ili kuongeza mapato, kuimarisha huduma za kitaalamu na kuifanya taasisi hiyo kuwa kitovu cha umahiri katika sekta ya barabara nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Ametoa ushauri huo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Makao Makuu ya TANROADS jijini Dodoma, ambapo pia ameitaka taasisi hiyo kuhakikisha viongozi wake wakuu na watumishi wanaopaswa kuhamia Makao Makuu ya nchi wanakamilisha uhamisho wao ifikapo mwisho wa Agosti mwaka huu.

Mhandisi Kasekenya alisema maabara za kisasa zinazojengwa zinapaswa kutumika si tu kuhudumia mahitaji ya TANROADS, bali pia kutoa huduma za kitaalamu kwa sekta binafsi, taasisi za elimu na nchi jirani, hatua itakayoongeza mapato na kuiwezesha taasisi hiyo kujitegemea zaidi kifedha.

"Tunapoelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni muhimu taasisi za umma kushirikiana na sekta binafsi. TANROADS ina nafasi ya kuwa kituo cha umahiri kwa kutumia maabara hizi za kisasa kutoa huduma za kitaalamu ndani na nje ya nchi," alisema.

Alisema ushirikiano huo utaongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kupitia ubadilishanaji wa uzoefu na teknolojia, huku ukiifanya TANROADS kuwa taasisi yenye ushindani katika utoaji wa huduma za upimaji wa vifaa vya ujenzi wa barabara.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Naibu Waziri alisema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji baada ya kupata maelezo kutoka kwa mshauri elekezi wa Serikali, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), pamoja na TANROADS.

Alisema jengo la maabara (Road Development Unit-RDU) linatarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa Agosti na kuanza kutumika mara moja, huku jengo kuu la Makao Makuu ya TANROADS likitarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu kutokana na kuchelewa kuwasili kwa baadhi ya vifaa maalumu vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.

"Baadhi ya viongozi tayari wameanza kufanya kazi katika jengo la maabara. Maelekezo yangu ni kwamba ifikapo mwisho wa Agosti viongozi wote wawe wamehamia Dodoma ili wafanye kazi pamoja na kuongeza ufanisi katika kufanya maamuzi," alisema.

Aidha, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa, akisema hatua hiyo inaimarisha uwezo wa taasisi za Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Awali, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, alisema mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya wakala huo wenye thamani ya Sh bilioni 49.72 umefikia asilimia 85, huku jengo kuu likiwa limekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.

Alisema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya CRJE East Africa Limited chini ya usimamizi wa Tanzania Building Agency (TBA), baada ya kuanza Februari 1, 2024, na kwa sasa kazi nyingi zilizobaki ni za umaliziaji.

Mhandisi Zuhura alisema ndani ya siku 14 zijazo mkandarasi anatarajia kukamilisha kazi muhimu zilizobaki katika jengo la maabara ili lianze kutumiwa na watumishi, huku takribani watumishi 220 wa TANROADS tayari wakiwa wamehamia Dodoma.

Aliongeza kuwa mradi huo umechangia matumizi ya malighafi zinazozalishwa nchini, kunufaisha viwanda vya ndani na kutoa ajira kwa Watanzania 211 pamoja na wataalamu wanane kutoka nje ya nchi.

Hata hivyo, alisema baadhi ya kazi zilichelewa kutokana na upatikanaji wa vifaa vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi, ingawa kwa sasa vifaa hivyo vimewasili na utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kasi.

Akihitimisha ziara hiyo, Mhandisi Kasekenya aliwataka watumishi wa TANROADS kuzingatia uadilifu na uwajibikaji katika matumizi ya maabara hizo ili kuhakikisha barabara zinazojengwa nchini zinakuwa na ubora unaotakiwa na kudumu kwa muda mrefu.

"Hatuwezi kuwa na maabara za kisasa halafu tukashuhudia barabara zikiharibika muda mfupi baada ya kujengwa. Uadilifu ndiyo msingi wa kulinda ubora wa kazi na thamani ya fedha za umma," alisema.







No comments:

Post a Comment