“KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050, TUNAYO MATARAJIO MAKUBWA NA MAWAKILI WA SERIKALI” – NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 17, 2026

“KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050, TUNAYO MATARAJIO MAKUBWA NA MAWAKILI WA SERIKALI” – NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab A. Katimba amesema kuwa, Serikali ina matarajio makubwa kwa Mawakili wa Serikali katika utekelezaji wa miradi mingi ya kimkakati itakayoliwezesha Taifa kutekeleza na kufikia Dira ya Taifa 2050.

Mhe. Katimba ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi wakati wa kufunga msimu wa tatu wa Mafunzo ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali, yaliyofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 15 hadi17 Julai, 2026.

Mhe. Katimba amesema kuwa, Serikali inatarajia kuwa na Mawakili wa Serikali wenye uwezo wa kuona mbali, kufikiri kimkakati, kutumia sheria kama nyenzo ya maendeleo, na kuhakikisha kuwa kila uamuzi wa Serikali unaimarisha uchumi, unalinda maslahi ya Taifa na unaongeza imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

“Tunahitaji Mawakili wa Serikali watakaohakikisha kila mkataba unalinda maslahi ya Taifa, unaongeza thamani ya fedha za umma, unaepusha migogoro, na unachangia maendeleo endelevu ya nchi yetu.” Amesema Mhe. Katimba

Aidha, Mhe. Naibu Waziri amewataka Mawakili wa Serikali kuyatumia maarifa waliyoyapata katika kuendelea kuboresha utendaji kazi wao ikiwemo kutoa ushauri wa Kisheria, kupekua na kusimamia mikataba, kushughulikia mashauri, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali na namna wanavyochangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Nina imani kubwa kuwa ninyi mliopo hapa mtakuwa sehemu ya kizazi hicho cha Mawakili wa Serikali kitakachoiwezesha Tanzania kufikia matarajio makubwa ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.” Amesema.


Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi amesema kuwa, Mawakili wa Serikali wamepata fursa ya kujadili na kujifunza masuala mbalimbali ya kimkakati kwa lengo la kuimarisha nafasi ya Mawakili wa Serikali katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

“Tunaamini maarifa na ujuzi walioupata kupitia mafunzo haya utawawezesha Mawakili wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ubunifu na ufanisi zaidi katika kulinda na kutetea maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
 Amesema Mhe. Maneno

Vilevile Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa mafunzo ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali yalijikita katika maeneo muhimu yanayohusu usimamizi wa majadiliano na mikataba ya kimkakati, usuluhishi wa migogoro, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), usimamizi wa vihatarishi vya kisheria (Legal risk management), pamoja na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) katika taaluma ya sheria.

Mhe. Maneno alitumia fursa hiyo, kuwasisitiza Mawakili wa Serikali kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA) kwa mwaka 2026, katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Amewataka Mawakili wa Serikali kuendelea Kusoma na Kutafakari kwa kina Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Mama Samia( Mama Samia Doctrine of Law) ili kuelewa dira ya uongozi na maendeleo ya Taifa, pamoja na kuongeza kasi na ufanisi katika uchakataji wa masuala ya kisheria, hususan upekuzi na uandaaji wa mikataba, bila kuathiri ubora wa kazi na kwa kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni, miongozo na maslahi ya Taifa.

Mhe. Maneno ameeleza kuwa Kauli mbiu ya mafunzo ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali 2026, "Repositioning State Attorneys for Strategic Legal Leadership in Realizing Tanzania Development Vision 2050," imeendelea kuwakumbusha Mawakili wa Serikali wajibu wao wa kujiendeleza kitaaluma ili waendelee kuwa nguzo muhimu katika kusimamia utawala wa sheria, kulinda rasilimali za umma, na kutoa ushauri wa kisheria unaochochea maendeleo endelevu ya Taifa.

Mawakili wa Serikali kutoka Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa (RS & LGAs) wameshiriki Mafunzo ya Bespoke 2026 yaliyofanyika kwa siku 3 kuanzia tarehe 15 hadi 17, 2026 Jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment