MBUNGE LUKUMAY ATEKELEZA AHADI, AWALETA WATAALAM WA AFYA KUTOKA UJERUMANI ARUMERU MAGHARIBI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 20, 2026

MBUNGE LUKUMAY ATEKELEZA AHADI, AWALETA WATAALAM WA AFYA KUTOKA UJERUMANI ARUMERU MAGHARIBI



Na Mwandishi Wetu, Arumeru


Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lembulung Lukumay, ametekeleza ahadi yake ya kuwaleta wataalamu na wafadhili wa afya kutoka Ujerumani kwa lengo la kuimarisha huduma za afya na kusaidia makundi yenye uhitaji katika jimbo hilo.

Ujumbe huo unaoongozwa na Dkt. Ursula umeanza ziara ya siku tano katika Arumeru Magharibi, ambapo utatembelea shule, vituo vya huduma za afya na maeneo yenye watoto wenye mahitaji maalumu ili kutathmini namna ya kushirikiana katika kuboresha huduma, hususan za afya ya kinywa na meno.

Mara baada ya kuwasili nchini, Dkt. Lukumay aliwatambulisha wageni hao kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kabla ya kuanza ziara rasmi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jimbo.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Dkt. Lukumay alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni na baada ya uchaguzi ya kutumia diplomasia ya maendeleo kuvutia wadau wa kimataifa watakaoshirikiana na wananchi wa Arumeru Magharibi katika kuboresha sekta ya afya.

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, siku ya kwanza ujumbe huo ulianza kwa kutembelea Shule ya Msingi Ngaramtoni, huku ukitarajiwa kuendelea na ziara katika maeneo mengine kwa siku zilizobaki.

Ziara hiyo pia imeelezwa kuwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Arumeru Magharibi na wadau wa maendeleo kutoka Ujerumani, ambapo wataalamu hao watapata fursa ya kujionea mahitaji yaliyopo na kubaini maeneo ya ushirikiano wa muda mrefu.

Wananchi wa Arumeru Magharibi wanatarajia ujio wa wataalamu hao utakuwa chachu ya kuimarisha huduma za afya na kufungua fursa zaidi za maendeleo kupitia ushirikiano wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment