NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Baraza la Famasi limeanzisha mkakati wa kuimarisha ushirikiano na wahariri na waandishi wa habari nchini kwa kuwajengea uelewa kuhusu majukumu yake, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu huduma za dawa na usimamizi wa taaluma ya famasi ili kulinda afya ya jamii.
Akifungua semina ya uhamasishaji kwa wahariri na waandishi wa habari, leo Julai 1, 2026 Jijini Dar es Salaam, Msajili wa Baraza la Famasi, Mfamasia Boniface Magige, amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na umuhimu wa kupata huduma za kifamasia kutoka katika maeneo yaliyosajiliwa na mamlaka husika.
Amesema licha ya Baraza la Famasi kuanzishwa mwaka 2011 chini ya Sheria ya Famasi, Sura ya 311, bado wadau wengi wakiwemo waandishi wa habari na wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusu kazi na majukumu yake katika kusimamia na kudhibiti taaluma ya famasi nchini.
"Kutokana na hali hiyo, Baraza limeona ni muhimu kukutana na wahariri pamoja na waandishi wa habari ili kuwajengea uelewa mpana kuhusu majukumu yake na kuimarisha ushirikiano utakaowezesha utoaji wa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu masuala ya usimamizi wa taaluma ya famasi kwa manufaa ya umma," amesema Magige.
Ameeleza kuwa Baraza la Famasi ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya yenye jukumu la kuhakikisha huduma za kifamasia nchini zinatolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maadili ya taaluma.
Magige amesema kupitia ushirikiano na vyombo vya habari, Baraza linatarajia kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu kuhusu umuhimu wa kununua dawa kutoka katika maduka na vituo vya kutolea huduma za dawa vilivyosajiliwa, ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya dawa kutoka maeneo yasiyotambulika.
Aidha, amesema semina hiyo pia inalenga kujadili namna bora ya kushirikiana katika kuhakikisha majengo yote yanayohifadhi, kusambaza na kutoa huduma za dawa yanazingatia matakwa ya sheria na kutoa huduma zinazokidhi viwango vilivyowekwa.
Kwa mujibu wa Magige, malengo ya semina hiyo ni pamoja na kutoa elimu kuhusu kazi na majukumu ya Baraza la Famasi, kuwaelimisha waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Famasi, kanuni na miongozo ya usimamizi wa taaluma hiyo, pamoja na kukumbushana wajibu wa kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa.
Pia amesema semina hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Baraza la Famasi na vyombo vya habari ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa taaluma ya famasi, sambamba na kupokea maoni ya wadau yatakayosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na Baraza.
Magige amesema washiriki watapata fursa ya kusikiliza mada mbalimbali zitakazowasilishwa na sekretarieti ya Baraza la Famasi, huku akieleza kuwa matarajio ni kuona waandishi wa habari wanakuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa na umuhimu wa kupata huduma za kifamasia katika maeneo yaliyosajiliwa na kusimamiwa na Baraza.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya usimamizi wa taaluma ya famasi na ulinzi wa afya ya wananchi yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya Baraza la Famasi, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla.








No comments:
Post a Comment