
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb)(katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Fedha wanaoshiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea banda la wizara hiyo.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), akipokea mfuko wenye vipeperushi vyenye taarifa mbalimbali za Benki Kuu ya Tanzania kutoka kwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayesimamia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dkt. Rahma Salim Mahfoudh, wakati alipotembelea banda la benki hiyo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb)(kulia), akisikiliza maelezo ya kutoka kwa Mkuu wa Sehemu ya Mafunzo ya Muda Mfupi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Bi. Dorah Chenyambuga (Kushoto), wakati alipotembelea banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb)(kulia), akisikiliza maelezo ya kutoka kwa Afisa Utumishi Mkuu kutoka Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Fedha, Bi. Dorothea Charles, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb)(kulia), akisikiliza maelezo ya kutoka kwa Afisa Msimamizi wa Mali za Serikali kutoka Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bi. Grace Matagi, wakati alipotembelea banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)
Na. Chedaiwe Msuya na Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 tayari unaonekana kwa vitendo kupitia kazi zinazofanywa na idara na taasisi mbalimbali za Wizara ya Fedha, huku akiwapongeza watumishi kwa namna walivyojipanga kuonesha mchango wao katika kufanikisha malengo ya taifa.
Mhe. Luswetula amesema hayo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, yenye kaulimbiu ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania”.
Alisema kuwa Idara na taasisi mbalimbali za Wizara ya Fedha zimekuwa zikifanya vizuri katika maonesho hayo hususan katika kuwasilisha elimu na taarifa mbalimbali na yanaonesha kwa dhahiri mwelekeo wa Serikali wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Nimefarijika sana kwa namna Wizara ilivyojipanga katika Maonesho haya, mabanda mengi katika jengo hili la Wizara yote yanaonesha namna yanavyokwenda kutimiza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na yamebeba mwelekeo huo wa kuijenga Tanzania kuelekea uchumi wa kipato cha juu," alisema Mhe. Luswetula.
Aidha, Mhe. Luswetula alipongeza hatua ya Wizara ya Fedha ya kuendelea kutumia mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa majukumu yake, akisema mabadiliko hayo yanaondoa matumizi yasiyo ya lazima ya karatasi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, ambapo hatua hio inaonesha ubunifu mkubwa na matumizi ya teknolojia katika kiwango cha juu, jambo linaloiwezesha Wizara kwenda sambamba na viwango vya kimataifa.
Mhe. Luswetula alisema Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji kupitia maboresho mbalimbali ya mifumo na huduma.
"Napenda kuwalika wafanyabiashara na wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini Tanzania waje wawekeze, Serikali imeweka mazingira wezeshi na vivutio mbalimbali vinavyowawezesha kufanya biashara katika mazingira bora, haya yote yanafanyika kwa lengo la kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inafikiwa" alisema Mhe. Luswetula.

No comments:
Post a Comment