Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limefungua dirisha la udahili kwa ngazi za astashahada na stashahada, huku likitoa huduma mbalimbali kwa wananchi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Hayo yamebainishwa leo Julai 2, 2026 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa NACTVET Dora Tesha, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la baraza hilo kwenye Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Amesema ushiriki wa NACTVET katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kwa umma, wateja na wadau mbalimbali kuhusu majukumu ya baraza hilo, hususan katika kusimamia utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Ameeleza kuwa wananchi wanaotembelea banda la NACTVET wanapata taarifa sahihi kuhusu vyuo vinavyosimamiwa na baraza, programu zilizoidhinishwa pamoja na utaratibu wa kufanya maombi ya kujiunga na kozi mbalimbali za cheti, astashahada na stashahada.
“Kwa sasa tumefungua dirisha la udahili kwa ngazi ya astashahada na stashahada. Tunawakaribisha wanafunzi, wazazi na walezi kufika katika banda letu ili kupata maelekezo sahihi kuhusu vyuo na programu ambazo zimeidhinishwa na baraza,” amesema.
Pamoja na huduma za udahili, amesema NACTVET pia inatoa maelekezo kwa watu wanaotaka kuanzisha vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, ikiwemo hatua za kufuata ili kusajili taasisi hizo.
Katika hatua nyingine, NACTVET imewatambulisha wanafunzi wanaosoma mkondo wa amali katika shule za sekondari, ambao wanashiriki kuonesha ujuzi mbalimbali wa vitendo katika maonesho hayo.
Amesema mkondo huo wa amali ulianzishwa kufuatia maboresho ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa vitendo wakiwa bado katika elimu ya sekondari.
“Lengo ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi mapema, ili wanapohitimu wawe na uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa na kutenda kazi mbalimbali kwa ufanisi,” amesema.
NACTVET imewaalika wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata huduma, elimu na kushuhudia uwezo wa wanafunzi wa mkondo wa amali katika kazi mbalimbali za ufundi na stadi za maisha.
Daudi Elias Mwasi ni Mwanafunzi wa Mkondo Amali Fani ya Ujenzi, Shule ya Sekondari ya Ufundi Bwiru na Careen Jonathan Maki Mwanafunzi Mkondo wa Amali - Fani ya Umeme, Shule ya Sekondari Baobab wamesema kupitia uanzishwaji mkondo wa amali kwasasa wameweza kujijenga ipasavyo katika kuhakikisha wanaonesha ujuzi walionao na kuwa tayari kupambana na soko la ajira linavyokwenda kwasasa.






No comments:
Post a Comment