NACTVET YAHAMASISHA ELIMU YA AMALI SABASABA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 6, 2026

NACTVET YAHAMASISHA ELIMU YA AMALI SABASABA



Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) imewataka wazazi, walezi na wadau wa elimu nchini kuhamasika kuwapeleka watoto kwenye mafunzo ya amali, ikieleza kuwa elimu hiyo inawajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kutekeleza kazi kwa vitendo.


Wito huo umetolewa leo Juni 06,2026 katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ambapo NACTVET inashiriki kwa mara nyingine kwa lengo la kusogeza huduma zake karibu na wananchi pamoja na kutoa elimu kuhusu uanzishwaji na usimamizi wa taasisi za elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.


Akizungumza katika banda la taasisi hiyo, Katibu Mtendaji wa NACTVET Dkt. Mwajuma   Lingwanda amesema wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kuuliza maswali na kupata huduma mbalimbali zinazopatikana katika ofisi za baraza, ikiwemo ushauri wa namna ya kuanzisha taasisi za elimu ya ufundi, kupata taarifa kuhusu uthibitishaji wa vyeti na huduma nyingine za kiutawala.


Amesema mwitikio wa wananchi katika banda hilo umeendelea kuwa mkubwa, huku rejesta ya wageni ikionyesha kuwa watu wengi tayari wamefika kupata huduma na taarifa walizokuwa wakizihitaji.

“Tunawakaribisha wananchi wote kutumia fursa ya maonesho haya kufika katika banda letu, kupata taarifa sahihi na huduma mbalimbali zinazotolewa na NACTVET. Pia tunaomba waliotembelea waendelee kuwafikishia wengine ujumbe kuwa bado tupo hapa Sabasaba na tunaendelea kuwahudumia,” amesema.


Mbali na huduma za ushauri na uthibitishaji wa vyeti, NACTVET imetumia maonesho hayo kuonesha umuhimu wa elimu ya amali kwa vitendo kupitia wanafunzi kutoka katika baadhi ya taasisi zinazotoa mafunzo hayo.


Wanafunzi hao wamekuwa wakionesha ujuzi mbalimbali walioupata darasani, hali inayodhihirisha uwezo wa elimu ya amali kuwajenga vijana wanaoweza kuelewa walichofundishwa na kukitekeleza katika mazingira halisi ya kazi.


Kwa mujibu wa NACTVET, mafunzo ya amali yana mchango mkubwa katika kutengeneza nguvu kazi yenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya uzalishaji na maendeleo ya taifa.


“Tulichokileta hapa ni baadhi tu ya fani zilizopo. Fani ni nyingi, lakini tumetoa mfano wa maeneo machache ili wananchi waone uwezo wa vijana wetu. Inawezekana mwakani tukapanua zaidi na kuonesha fani nyingine,” amesema.


Hatua hiyo inalenga kuongeza idadi ya taasisi zinazotoa mafunzo ya ufundi stadi nchini, sambamba na kuwapa vijana wengi zaidi nafasi ya kupata ujuzi unaowawezesha kuajirika au kujiajiri.

No comments:

Post a Comment