NCHI ZA SADC ZASHAURIWA KUJENGA VIWANDA ILI KUKUZA AJIRA KWA WANAWAKE NA VIJANA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 29, 2026

NCHI ZA SADC ZASHAURIWA KUJENGA VIWANDA ILI KUKUZA AJIRA KWA WANAWAKE NA VIJANA

Baadhi ya Washiriki wa Wiki ya Tisa ya Viwanda kutoka nchi wanachama wa SADC wakifuatilia mojawapo ya mjadala kuhusu masuala ya madini uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), Durban, Afrika Kusini.
Meneja wa Mawasiliano, Masoko na Mahusiano wa Benki ya Maendeleo - TIB, Bw. Allan Chonjo akitoa maelezo kuhusu bidhaa na huduma zinazotolewa na Benki hiyo kwa baadhi ya wadau waliotembelea Banda la Tanzania, pembezoni mwa Mkutano wa Wiki ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini.
Afisa Sheria kutoka Tume ya Ushindani (FCC) akielezea ubora na faida za mkonge unaozalishwa Tanzania kwa mdau aliotembelea Banda la Tanzania, pembezoni mwa Mkutano wa Wiki ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini.
Baadhi ya Washiriki kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali wakiwa katika picha ya Pamoja baada ya Mkutano wa Wiki ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini.

Na. Ramadhani Kissimba, Durban.


Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeshauriwa kuwekeza zaidi katika maendeleo ya viwanda na miundombinu ili kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa ukanda wa SADC.

Ushauri huo umetolewa jijini Durban nchini Afrika Kusini na Meneja wa Utafiti na Biashara wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Dkt. Hilderbrand Shayo, kando ya Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC unaoendelea nchini humo.

Alisema kuwa uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa utasaidia kuwainua wanawake na vijana kiuchumi, kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania na kuongeza mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mkutano na maonesho hayo, Dkt. Shayo alisema matukio hayo yanaendana na vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania, hususan katika sekta za madini, kilimo, bidhaa za afya pamoja na maendeleo ya miundombinu na ubunifu, ambazo ni maeneo yanayopewa kipaumbele katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

"Ushiriki wa Tanzania katika Wiki ya Viwanda ya SADC una umuhimu mkubwa kwa sababu mkutano huu umejikita katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta za madini, kilimo na bidhaa za afya, sambamba na maendeleo ya miundombinu na ubunifu na ni maeneo muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu," alisema Dkt. Shayo.

Aidha, alisema kuwa maonesho hayo yamefungua fursa mpya za uwekezaji, ambapo wawekezaji kutoka nchi mbalimbali wameonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania kutokana na mazingira mazuri ya biashara pamoja na nafasi ya kimkakati ya nchi hiyo kama lango la biashara kupitia Bandari ya Dar es Salaam inayohudumia nchi nyingi wanachama wa SADC.

Dkt. Shayo, aliongeza kuwa ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo umeiwezesha nchi kuzitangaza fursa zake za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya ukanda wa SADC.

Sambamba na hilo, Dkt. Shayo alizishauri taasisi za fedha zilizoshiriki katika mkutano huo, ikiwemo Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Benki ya Exim, BADEA, Nedbank na taasisi nyingine za kifedha, kuimarisha ushirikiano katika kutafuta mitaji na fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na uwekezaji nchini Tanzania.

"Taasisi za fedha zilizoshiriki katika maonesho haya zina nafasi kubwa ya kushirikiana katika kuhamasisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na uwekezaji ambayo itachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania," alisema Dkt. Shayo

Akizungumzia sekta ya madini, Dkt. Shayo alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mengi ya kimkakati yanayohitajika duniani, hususan katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia.

Alisisitiza umuhimu wa kuyachakata madini hayo ndani ya nchi badala ya kuuza malighafi pekee, hatua ambayo itaongeza thamani ya bidhaa, kuzalisha ajira zaidi, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani.

Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda. Kwa Tanzania, ushiriki katika mkutano huo unaendelea kufungua fursa mpya za uwekezaji, masoko na ubia wa kifedha, huku ukiunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

No comments:

Post a Comment