NEEC YALETA ELIMU YA MITAJI KARIBU NA WANANCHI RUKWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 13, 2026

NEEC YALETA ELIMU YA MITAJI KARIBU NA WANANCHI RUKWA

Mafunzo ya utoaji wa elimu kuhusu fursa za mitaji kupitia mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi yanaendelea kufanyika katika Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, yakilenga kuwaongezea wananchi uelewa kuhusu fursa za kupata mitaji na huduma za maendeleo ya biashara ili kukuza shughuli za kiuchumi.

Mgeni rasmi katika mafunzo hayo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Mheshimiwa Prof. Riziki Silas Shemdoe, ambaye ameambatana na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa na mwenyeji wa shughuli hiyo, Mheshimiwa Jackline Mzindakaya, pamoja na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC), Bw. Gwakisa Bapala.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Prof. Shemdoe amewataka wananchi kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na Serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha na uwezeshaji ili kujenga uchumi imara kupitia ujasiriamali, kilimo, biashara na shughuli nyingine za uzalishaji. Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayo warahisishia wananchi kupata mitaji na huduma za kifedha kwa ajili ya maendeleo yao.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Jackline Mzindakaya amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Rukwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo na kutumia elimu wanayoipata kuboresha miradi yao ya kiuchumi. Amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kuwaunganisha wananchi na taasisi zinazotoa huduma za kifedha na maendeleo ya biashara.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa NEEC, Bw. Gwakisa Bapala, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa NEEC wa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu fursa za mitaji, namna ya kuandaa miradi yenye sifa za kufadhiliwa na matumizi sahihi ya mikopo kwa maendeleo endelevu ya biashara na uwekezaji.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji wananchi kiuchumi wanaowasilisha huduma na fursa mbalimbali za mitaji, wakiwemo SELF Microfinance Fund (SELF MF), CRDB Bank, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Agricultural Inputs Trust Fund (AGITF), Azania Bank pamoja na PASS Trust.

Mafunzo hayo yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wananchi, Serikali na taasisi za uwezeshaji, huku yakitarajiwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa zilizopo na kuchochea ushiriki mkubwa zaidi katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment