PROF. NOMBO: UJUZI WA KISASA NI NGUZO YA VIWANDA NA TEKNOLOJIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 31, 2026

PROF. NOMBO: UJUZI WA KISASA NI NGUZO YA VIWANDA NA TEKNOLOJIA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,akizungumza Julai 31, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao cha Kamati Elekezi ya Programu ya Pili ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ II)


Na.Mwandishi Wetu.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema Programu ya Pili ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ II) ni hatua ya kimkakati inayolenga kuongeza ajira zenye tija na kuimarisha ustawi wa jamii.

Akizungumza Julai 31, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao cha Kamati Elekezi ya Programu hiyo, Prof. Nombo amesema kuwa programu hiyo inalenga kuzalisha rasilimali watu wenye umahiri wa kisasa kwa sekta za viwanda, teknolojia, ubunifu na sekta binafsi, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Prof. Nombo amebainisha kuwa Programu imeandaliwa katika misingi ya Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kuendeleza Ujuzi, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023, pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa matokeo makuu yanayotarajiwa ni kuongeza fursa za mafunzo kwa vijana wasio na ajira na wanaotoka katika mazingira magumu, kuimarisha mfumo wa kusimamia Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), na kushirikisha sekta binafsi katika kuboresha ubora wa mafunzo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Programu ya Pili ya Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi, Dkt. Erick Mgaya, amesema utekelezaji wa Programu hiyo ni wa miaka sita wenye thamani ya Shilingi bilioni 780 sawa na Dola za Kimarekani milioni 300 unatarajiwa kunufaisha zaidi ya Watanzania milioni moja.

Amefafanua kuwa programu hii inatekelezwa na Taasisi 19 pamoja na wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, pamoja na taasisi za mafunzo zikishirikiana na Sekta binafsi.

No comments:

Post a Comment