
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Julai 20, 2026 mkoani Kigoma ambapo atatembelea, atazindua na kuweka jiwe la msingi katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Wizara ya Uchukuzi mkoani humo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Julai 19, 2026 mkoani Kigoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu hafla hiyo ambayo itajumuisha uzinduzi wa meli nne za mizigo, uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa(SGR) kipande cha sita kutoka Tabora hadi Kigoma pamoja na kutembela na kukagua uboreshaji wa Bandari ya Kigoma.
Prof. Makame amesema kuwa, miradi hiyo ya kimkakati inatekelezwa kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayohitaji nchi kuwa na usafiri fungamanishi kwa njia zote za usafirishaji, pia utekelezaji wa miradi hiyo utaendelea kuuwezesha mkoa huo kuwa lango muhimu la Tanzania kuelekea masoko ya ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika ya Kati.
“Mkoa wa Kigoma una fursa nyingi za sekta ya uchukuzi kwa kuwa unaunganishwa na ziwa Tanganyika, nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia hivyo, utekelazaji wa miradi hii utawezesha mkoa huu na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuhudumia masoko makubwa ya nchi hizo na kuimarisha ushoroba wa kati”, amesema Prof. Mbarawa.
Akielezea faida za miradi hiyo amesema kuwa, uzinduzi wa meli nne za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 2000 kila moja utaongeza uwezo wa Tanzania kusafirisha mizigo moja kwa moja kwenda nchi jirani kupitia Ziwa Tanganyika, pia nchi itanufaika na ongezeko la mzigo katika bandari za Ziwa Tanganyika.
Prof. Mbarawa amesema kuwa maboresho ya Bandari ya Kigoma yataziwezesha meli hizo mpya na zile zilizopo kufanya safari katika mkoa huo na bandari zilizopo kwenye mikoa mingine na nje ya nchi.
Akizungumza kuhusu mradi wa SGR, amesema kuwa kipande cha reli chenye urefu wa kilomita 506 kitakapokamilika, kitaunganisha Kigoma na mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Morogoro, na Dar es Salaam ambapo mizigo inayoingia na kutoka nchini hususan kupitia Bandari ya Dar es Salaam itaweza kusafirishwa kwa reli ya kisasa kwenda Kigoma na kuendelea katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia.
Aidha, reli hiyo itakapokamilika itawezewesha usafiri kati ya Kigoma na Dar es salaam kutumia takribani muda wa saa 8 pekee.
Prof. Mbarawa ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wote kushuhudia hafla hiyo hasa kwa wale wanaoishi mkoani Kigoma kwani ndiyo wanufaika wakubwa wa miradi hiyo.


No comments:
Post a Comment