SADC YASISITIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUONGEZA THAMANI YA MADINI NA BIDHAA KATIKA UKANDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 30, 2026

SADC YASISITIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUONGEZA THAMANI YA MADINI NA BIDHAA KATIKA UKANDA


Mchumi kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Jesca Mboho, akifuatilia kwa makini mijadala inayoendelea katika Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Industrialisation Week), unaofanyika jijini Durban, Afrika Kusini.

Meneja wa Utafiti na Biashara kutoka Benki ya Maendeleo (TIB), Dkt.Hilderbrand Shayo (kushoto), akiwa katika mazungumzo na Afisa Usimamizi Mkuu wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Emerensiana Nyanda (katikati), pamoja na Mchumi kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Jesca Mboho, mara baada ya kumalizika kwa vikao vya Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaoendelea jijini Durban, Afrika Kusini.

Meneja wa Utafiti na Biashara wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Dkt. Hilderbrand Shayo, akitoa mchango wake wakati wa mijadala katika Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Industrialisation Week), unaoendelea jijini Durban, Afrika Kusini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo (TIB), Bw. Deogratius Kwiyukwa (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Industrialisation Week), unaofanyika jijini Durban, Afrika Kusini.

Afisa Sheria kutoka Tume ya Ushindani (FCC), Bw. Goerge Chananga akielezea ubora, matumizi na fursa za kiuchumi za mkonge unaozalishwa nchini Tanzania kwa mmoja wa wadau waliotembelea Banda la Tanzania, pembezoni mwa Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC (SADC Industrialisation Week 2026), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha-Durban)


Na. Ramadhani Kissimba, Durban


Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeshauriwa kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati ya pamoja itakayochochea maendeleo ya viwanda pamoja na kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa zinazozalishwa katika ukanda huo.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Bw. Deogratius Kwiyukwa, kando ya Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa SADC (SADC Industrialisation Week) unaoendelea jijini Durban, Afrika Kusini.

Akizungumza kuhusu mijadala ya mkutano huo, Bw. Kwiyukwa alisema moja ya ajenda kuu ni namna nchi wanachama zitakavyowekeza katika viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya ukanda wa SADC, hususan madini ya kimkakati (critical minerals), badala ya kuendelea kuuza nje ya nchi madini hayo yakiwa katika hali ghafi.

“Jambo kubwa lililojadiliwa ni namna ya kuyaongezea thamani madini ya kimkakati katika nchi yanakopatikana madini hayo ndani ya ukanda huu kabla ya kuuzwa katika masoko ya nje,” alisema Bw. Kwiyukwa.

Alibainisha kuwa mkutano huo umefungua fursa mpya za ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama, zikiwemo fursa za kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia kufanikisha malengo ya maendeleo ya viwanda na uchumi yaliyowekwa na SADC.

Aidha, Bw. Kwiyukwa alizishauri nchi wanachama kuhakikisha sera na mipango yao ya maendeleo inaendana na dira na mikakati ya SADC ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye manufaa ya pamoja kwa ukanda huo.

Kwa upande wa Benki ya Maendeleo (TIB), Bw. Kwiyukwa alisema taasisi hiyo imeshiriki katika mkutano huo kwa lengo la kutafuta fursa za kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha ndani ya ukanda wa SADC ili kuunganisha mitaji kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo.

“Kama TIB, tumeshiriki katika mkutano huu kwa lengo la kujenga ushirikiano na taasisi nyingine za kifedha ili kuunganisha mitaji itakayowezesha kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na nchi wanachama wa SADC,” aliongeza Bw. Kwiyukwa.

Vilevile, Bw. Kwiyukwa alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kutafsiri kwa vitendo maazimio ya mkutano huo kwa kuwekeza katika sekta zinazozalisha ajira, hususan kwa vijana, ili waweze kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zinazopatikana ndani ya ukanda wa SADC.

Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa SADC umewakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za kifedha, wataalamu na wadau wa maendeleo kutoka nchi wanachama wa SADC. Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kukuza Viwanda Imara, Endelevu na Jumuishi kupitia Maendeleo ya Miundombinu, Mageuzi ya Kilimo na Madini kwa Ajili ya Dunia Yenye Haki.”

Kwa ujumla, mijadala ya Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC jijini Durban imeweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza thamani ya rasilimali za madini na bidhaa nyingine kabla ya kuuzwa nje, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda, miundombinu na miradi ya maendeleo. Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza ushindani wa uchumi wa ukanda wa SADC, kuvutia uwekezaji, kuimarisha biashara ya ndani ya ukanda na kuzalisha ajira zaidi, hususan kwa vijana.

No comments:

Post a Comment