TADB YAFIKISHA MITAJI YA ZAIDI YA SH. TRILIONI 1, YAIMARISHA USALAMA WA CHAKULA NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 30, 2026

TADB YAFIKISHA MITAJI YA ZAIDI YA SH. TRILIONI 1, YAIMARISHA USALAMA WA CHAKULA NCHINI


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ( TADB), Frank Nyabundege, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma Julai 30, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa benki hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imefikia mtaji na fedha za maendeleo zinazozidi Sh trilioni 1.04, huku asilimia 73.6 ya mikopo yote iliyotolewa na benki hiyo ikitolewa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Nyabundege ameyasema hayo leo Julai 30, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO kuhusu utekelezaji wa TADB kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na mwelekeo wa mwaka 2026/2027.

Amesema TADB ilianzishwa kama benki ya Serikali kwa lengo la kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata huduma za kifedha, huku ikilenga kubadili kilimo kutoka cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara chenye tija na ushindani.

Nyabundege amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha uwezo wa benki hiyo kupitia ongezeko la mtaji, ambapo kabla ya mwaka 2021 TADB ilikuwa na mtaji wa Sh bilioni 60 pekee.

Amefafanua kuwa mwaka 2021 Serikali iliongeza mtaji wa Sh bilioni 208 na kufanya mtaji kufikia Sh bilioni 268, mwaka 2024 ikaongeza Sh bilioni 174.16 kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na kufikisha mtaji Sh bilioni 442.16, huku mwaka 2025 ikiongeza Sh bilioni 10 na kufanya mtaji kufikia Sh bilioni 452.16.

Mbali na mtaji huo, amesema TADB imefanikiwa kuvutia mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 445.6, Mfuko wa Dhamana (SCGS) wenye Sh bilioni 108.4 pamoja na fedha zinazosimamiwa kwa niaba ya Serikali zenye thamani ya Sh bilioni 36.54.

Nyabundege amesema uwekezaji huo umeiwezesha benki kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo, ambapo asilimia 73.6 ya mikopo yote imetolewa kati ya mwaka 2022 na 2025, kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema mchango wa TADB umeonekana katika kuimarisha usalama wa chakula nchini kupitia ufadhili wa kilimo, ununuzi wa mitambo na pembejeo, hatua iliyochangia taifa kufikia kiwango cha kujitosheleza kwa chakula cha asilimia 130 mwaka 2025.

Aidha, amesema benki hiyo imefadhili ujenzi wa maghala, vihenge, nyumba za baridi na miundombinu ya usafirishaji ili kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, sambamba na kuwekeza katika minyororo ya thamani iliyoboreshwa ili kuongeza masoko, kuleta utulivu wa bei na kuongeza kipato cha wakulima.

Katika mwelekeo wa mwaka 2026/2027 kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Nyabundege amesema TADB itaendelea kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kukuza matumizi ya teknolojia, kuwawezesha vijana na wanawake, kuimarisha kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza thamani ya mazao kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.



No comments:

Post a Comment