‎SEKTA BINAFSI WATAJWA KUWA WADAU MUHIMU KATIKA KUFANIKISHA DIRA 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 28, 2026

‎SEKTA BINAFSI WATAJWA KUWA WADAU MUHIMU KATIKA KUFANIKISHA DIRA 2050

‎Na Mwandishi Wetu - Dodoma
‎Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa Viongozi na watumishi wa Mkoa wake kubadilisha mitazamo yao juu ya sekta binafsi kwani ni wadau muhimu wa kufanikisha Dira ya Maendeleo 2050 kwa kuwa, mtazamo wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sekta hizo, ni kuwawezesha watanzania kumiliki uchumi wao wenyewe kupitia kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani.
‎Senyamule ametoa Wito huo Julai 28,2026 wakati wa kufunga kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Mkoa, kilichojadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Miradi ya maendeleo na Mpango wa Bajeti 2025/26 sambamba na maandalizi ya ‘Samia Day’ inayotarajiwa kufanyika Septemba, 2026.
‎“Katika kutekeleza Dira hii, tutaendelea kupokea wageni wengi kutoka nje ambao wanakuja kutumia fursa hiyo ambayo Serikali imeieleza kuwa, 70% ni sekta binafsi, mwekezaji kutoka nje atakuja na mtaji, teknolojia na sisi tutafaidika na kodi, ajira na mambo mengine, hivyo, tuhakikishe tunabadilisha mtazamo jinsi tunavyoiangalia sekta binafsi, tuone kama ni wadau wetu na wenzetu wa kufanikisha Dira 2050”.
‎Aidha, Mhe. Senyamule ameagiza Halmashauri zote za Mkoa wake kuhakikisha zinakamilisha Miradi yote ya mwaka wa fedha 2025/26 ambayo haijakamilika, ikamilike kabla ya mwezi Oktoba, 2026 pia amewataka kutoa fedha za mikopo ya 10% zilizobakia kwa vijana, wanawake na makundi maalum kama ilivyoelekezwa ambapo mpaka sasa zimeshatolewa kwa 98%.
‎Kwa upande mwingine, amewataka kuzingatia suala la Utawala bora kwa kufanya vikao vya kikanuni ikiwa ni pamoja na vikao vya Mabaraza ya Madiwani, Vikao vya Maendeleo ya Kata ambapo utekelezaji wake ni 100% ingawa kuna changamoto kwenye vikao vya maendeelo ya Vijiji kwani utekelezaji wake ni 70% hivyo, kuna 30% ya vijiji ambavyo havijatekeleza.
‎Vile vile, amewatangazia wananchi kuhusu maandalizi ya ‘Samia Day 2026’ kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kutoka ile ya mwaka 2025 ambapo wananchi zaidi ya Milioni 1.7 ambao ni takribani nusu ya idadi ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma katika ngazi ya Kata, walipata fursa ya kufahamu kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
‎Ameongeza kuwa, ‘Samia Day 2026’ itaboreshwa zaidi kutokana na Jitihada za Mhe. Rais kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yanayotarajiwa kufanyika nchini 2027 kwa ushirikiano na Mataifa ya Kenya na Uganda hivyo, siku hiyo itatumika kuhamasisha wananchi kuelewa juu ya mashindano hayo na kushiriki kikamilifu wakati utakapofika.

No comments:

Post a Comment