SERIKALI, BARRICK WAZINDUA MRADI WA SH. BILIONI 70 KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA ELIMU NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 2, 2026

SERIKALI, BARRICK WAZINDUA MRADI WA SH. BILIONI 70 KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA ELIMU NCHINI

SERIKALI imezindua rasmi Mradi wa Twiga Future Forward Education Program unaotekelezwa kwa ushirikiano na Barrick Tanzania, huku ikisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa katika sekta ya elimu ni nguzo muhimu ya kujenga uchumi wenye ushindani, kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na kuongeza tija katika maendeleo ya taifa.

Akizindua mradi huo Kibaigwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali imeendelea kuweka elimu katika vipaumbele vyake kwa kuimarisha miundombinu ya shule ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata mazingira bora ya kujifunzia na kufikia ndoto zake.

Amesema elimu ndiyo msingi wa maendeleo endelevu na kwamba uwekezaji katika madarasa, mabweni na miundombinu mingine ya shule ni hatua muhimu ya kuandaa kizazi chenye maarifa, stadi na maadili kitakachochochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.

"Elimu bora haiwezi kupatikana bila kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, hivyo uwekezaji katika sekta hiyo ni mkakati muhimu wa kukuza rasilimali watu nchini," amesema Profesa Shemdoe.

Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali na Barrick Twiga Minerals, zaidi ya Shilingi bilioni 70 zimetengwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za sekondari nchini, ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo.

Prof. Shemdoe amesema mafanikio ya mradi huo yametokana na mazungumzo yaliyofanyika kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold Corporation, Mark Bristow, yaliyowezesha kampuni hiyo kutoa msaada wa dola za Marekani milioni 30 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule nchini.

Katika kuhakikisha mradi huo unaleta matokeo yaliyokusudiwa, Waziri huyo amemuelekeza Katibu Mkuu wa TAMISEMI kuhakikisha fedha zilizobaki zinatumika kujenga bwalo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaigwa ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa miundombinu hiyo muhimu.

Aidha, ameiagiza timu ya Serikali inayoshughulikia majadiliano na Barrick kurejea mezani kujadili uwezekano wa kupata ufadhili mwingine wa dola milioni 30 au zaidi ili kuongeza kasi ya ujenzi wa madarasa na miundombinu mingine, ikiwa ni maandalizi ya ongezeko kubwa la wanafunzi litakalotokana na madarasa mawili ya elimu ya msingi kuhitimu kwa wakati mmoja mwaka 2028.

Prof. Shemdoe pia amezitaka halmashauri zote zinazotekeleza mradi huo kuusimamia kwa umakini, kuhakikisha wakandarasi wanazingatia viwango vya ubora na kuweka mfumo endelevu wa matengenezo ya miundombinu itakayojengwa.

Kadhalika, amewataka wakuu wa shule, walimu, wazazi na wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu hiyo ili iweze kuendelea kunufaisha wanafunzi wa sasa na vizazi vijavyo.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi ukamilike ifikapo Agosti 30 mwaka huu, ili kutoa nafasi ya kuanza kwa awamu ya tatu bila kuchelewa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Barrick Tanzania, Melkiory Ngido, amesema kampuni imepokea maelekezo ya Serikali kuhusu mahitaji ya ziada ya miundombinu kwa ajili ya wanafunzi watakaomaliza elimu ya msingi mwaka 2028 na kwamba itayafanyia kazi kupitia kamati inayosimamia utekelezaji wa mradi huo.

Amesema hadi sasa Barrick imeshatumia dola milioni 20 katika utekelezaji wa mradi huo, huku dola milioni 10 zilizobaki zikitarajiwa kuelekezwa katika maeneo yatakayopangwa kwa pamoja na Serikali kulingana na mahitaji yaliyopo.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi huo, utakapokamilika utahusisha ujenzi wa madarasa 1,090 yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 54,500, mabweni 270 yatakayochukua wanafunzi 21,600, pamoja na matundu ya vyoo 1,640 yatakayohudumia wanafunzi 49,200 katika halmashauri zote za Tanzania Bara.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Atupele Mwambene, amesema mradi huo unalenga kuongeza uwezo wa shule za sekondari kupokea wanafunzi wengi zaidi, kupunguza msongamano madarasani, kuongeza nafasi za kuendelea na masomo hususan kidato cha tano na kuinua kiwango cha ufaulu.

Kwa upande wake, Afisa wa Barrick Tanzania, Penina Katuki, amesema uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 70 unaakisi dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kujenga mazingira bora, salama na rafiki kwa kujifunzia na kufundishia.

No comments:

Post a Comment