SERIKALI KUUNGANISHA MALINYI NA ULANGA KWA MIUNDOMBINU YA KISASA YA BARABARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 16, 2026

SERIKALI KUUNGANISHA MALINYI NA ULANGA KWA MIUNDOMBINU YA KISASA YA BARABARA


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kuanza kwa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja katika wilaya za Malinyi na Ulanga, mkoani Morogoro, kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa barabara ya Ifakara–Lupiro–Malinyi yenye urefu wa kilometa 112 kwa kiwango cha lami, pamoja na ujenzi wa Daraja la Fuluwa lenye urefu wa mita 100 na Daraja la Namahanga.

Akizungumza na wananchi wa Malinyi na Ulanga, Waziri Ulega amesema Serikali tayari imetenga fedha katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo inalenga kurahisisha uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya kilimo pamoja na madini.

"Niwahakikishie wananchi wa Malinyi na Ulanga kwamba ujenzi wa kilometa 112 kutoka Ifakara hadi Malinyi pamoja na madaraja mawili makubwa unaanza. Serikali inaanza kumlipa mkandarasi kwa kuwa maandalizi yote ya mradi yamekamilika," amesema Ulega.

Aidha, Waziri Ulega amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuunganisha halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro na makao makuu ya mkoa kupitia miundombinu bora ya barabara, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama na za uhakika za usafiri.

Pia, ametoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro kumsimamia kwa karibu mkandarasi anayetekeleza miradi hiyo ili kazi zifanyike usiku na mchana na zikamilike kwa wakati pamoja na kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa na kusisitiza kuondoa urasimu wowote unaoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega ameahidi kuendelea kufungua na kuboresha miundombinu ya Wilaya ya Malinyi kupitia ujenzi wa barabara ya Malinyi–Kilosa kwa Mpepo hadi Longo, ambayo itaiunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma.

Vilevile, amesema Serikali itajenga gati katika Wilaya ya Malinyi na kurejesha huduma ya kivuko ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Mlimba na Malinyi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufufua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo uliokuwa umesimama kwa muda mrefu, akieleza kuwa utekelezaji wake utachochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi wa Morogoro na mikoa jirani.

Naye Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dkt. Mecktridis Mdaku, amemshukuru Waziri wa Ujenzi kwa kutembelea wilaya hiyo, akisema ujio wake umeleta matumaini mapya kwa wananchi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za miundombinu ya usafiri na kukamilika kwa barabara na madaraja hayo kutarahisisha mawasiliano na utoaji wa huduma za kijamii katika wilaya za Malinyi na Ulanga.

No comments:

Post a Comment