SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA SEKTA YA AFYA, HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KULENGA KUWA KITOVU CHA UTALII WA MATIBABU AFRIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 22, 2026

SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA SEKTA YA AFYA, HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KULENGA KUWA KITOVU CHA UTALII WA MATIBABU AFRIKA



Na Boniphace John – Dodoma


Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa lengo la kuiwezesha kuwa Kijiji cha Utalii wa Matibabu (Medical Tourism Village) ndani ya kipindi cha miaka 10 ijayo, hatua inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Julai 22, 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya afya, kuvutia wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi na kuongeza mapato kupitia utalii wa matibabu.

Amesema pamoja na kuongeza mapato ya taifa, mpango huo utasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu ambayo sasa yanapatikana nchini.

Msigwa amesema Hospitali ya Benjamin Mkapa pia inatarajia kuanzisha Chuo cha Afya kitakachotoa mafunzo ya ngazi ya diploma ili kuongeza wataalamu wa afya wenye ujuzi unaohitajika katika utoaji wa huduma za kibingwa.

Ametaja baadhi ya miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa katika hospitali hiyo kuwa ni ujenzi wa Jengo la Matibabu ya Figo lenye thamani ya shilingi bilioni 44.9, ambapo Serikali ya Tanzania imechangia shilingi bilioni 16.9, huku Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ikichangia shilingi bilioni 28.17.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji wa Uloto (Bone Marrow Transplant Centre) pamoja na ujenzi wa Jengo la Saratani lenye thamani ya shilingi bilioni 32.

Msigwa amesema uwekezaji wa Serikali katika sekta ya afya unaendelea pia katika maeneo mengine nchini, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kigoma, ambapo shilingi bilioni 8 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD Complex), huku mradi ukiwa katika hatua za manunuzi ya kumpata mkandarasi.

Kwa upande wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 61.43 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa Uhuishaji wa Hospitali ya Muhimbili (Muhimbili Redevelopment Project) pamoja na ujenzi wa wodi binafsi. Alibainisha kuwa upembuzi yakinifu umekamilika na mkataba wa ujenzi uko tayari kuanza kutekelezwa.

Msigwa ameongeza kuwa Serikali imeomba Hazina kutoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitakavyosaidia kuboresha zaidi huduma za afya nchini.

Vilevile, amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ukarabati wa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), ukarabati wa jengo la upasuaji pamoja na ununuzi wa vifaa tiba (implants).

Amesema hadi sasa ukarabati wa jengo la OPD umefikia asilimia 36, huku taratibu za ununuzi wa vipandikizi zikiwa zimewasilishwa Hazina kwa ajili ya utekelezaji.


No comments:

Post a Comment