
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imetangaza orodha ya wanafunzi 1, 050 waliofanya vizuri zaidi katika mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2026 ambao watanufaika na ufadhili wa masomo ya vyuo vikuu kupitia Samia Scholarship.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 27,2026 jijini Dodoma , Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda huku akiongea kuwa wanafunzi 50 bora zaidi watapelekwa kusoma nje ya nchi katika fani za Akili Unde (Artificial Intelligence - AI), Data Science na teknolojia nyingine za kisasa.
"Mpango huu unatekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo unalenga kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) ili kujenga wataalamu watakaochochea maendeleo ya taifa", amesema.
Amesema katika wanafunzi hao, 1,000 watapata ufadhili wa kusoma katika vyuo vikuu vya ndani, huku 50 bora zaidi wakiandaliwa kwenda kusoma nje ya nchi katika fani za teknolojia zinazoibukia.
"Wanafunzi hao wamepatikana kutoka katika tahasusi za PCM (Physics, Chemistry and Mathematics), PCB (Physics, Chemistry and Biology), CBG (Chemistry, Biology and Geography), PMG (Physics, Mathematics and Geography), CBA (Chemistry, Biology and Agriculture) pamoja na PMC (Physics, Mathematics and Computer Science)", amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, wanafunzi watakaonufaika na ufadhili wa ndani wanapaswa kuomba udahili katika vyuo vikuu vya Tanzania kusomea shahada za Hisabati, Sayansi, Uhandisi au Tiba. Baada ya kupata nafasi ya masomo, watajaza fomu ya kujiunga rasmi na mpango wa Samia Scholarship na Serikali itagharamia masomo yao kwa asilimia 100.
Aidha, amesema majina ya wanafunzi wote waliochaguliwa yamewekwa kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuwataka wahitimu wa Kidato cha Sita kuyakagua na kufuata taratibu zilizowekwa ili kukamilisha mchakato wa kupata ufadhili huo.
Akizungumzia wanafunzi 50 bora zaidi, Waziri Mkenda amesema wameteuliwa kutoka katika tahasusi za PCM, PMG na PMC, ambazo zote zinahitaji uwezo mkubwa wa Hisabati ya Juu (Advanced Mathematics).
"Wanafunzi hao watapelekwa kusoma nje ya nchi katika fani za Artificial Intelligence, Data Science na teknolojia nyingine za kisasa zinazohitajika katika uchumi wa kidijitali", amesema.
Ameeleza kuwa uteuzi umefanyika kwa kuzingatia alama halisi za mtihani na si daraja la ufaulu pekee, kwani wanafunzi wengi wanaweza kuwa na daraja la "A" lakini wakatofautiana kwa idadi ya alama walizopata.
Profesa Mkenda amesisitiza kuwa Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika uwazi na uadilifu wa mchakato huo ili kulinda heshima ya Samia Scholarship, akibainisha kuwa mwanafunzi yeyote mwenye mashaka kuhusu kutokuwamo kwenye orodha anaweza kuwasiliana na Wizara kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa alama zake kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).
Pia amebainisha kuwa kati ya wanafunzi wote waliochaguliwa, asilimia 58 wametoka katika shule za serikali huku asilimia 42 wakitoka katika shule zisizo za serikali, akisisitiza kuwa uteuzi umezingatia ufaulu na vigezo vilivyowekwa bila kujali aina ya shule aliyosoma mwanafunzi.
Amewataka wanafunzi waliochaguliwa kutumia fursa hiyo kwa bidii na uzalendo, akieleza kuwa uwekezaji huo wa Serikali unalenga kuzalisha wataalamu watakaosaidia Tanzania kuimarisha ushindani katika sayansi, teknolojia na ubunifu duniani.






No comments:
Post a Comment