Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Oryx Tanzania imezindua kitabu cha Mwongozo wa Matumizi Salama ya Gesi ya LPG na kusaini mkataba wa ushirikiano wa miaka mitatu na Chama cha Skauti Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha elimu ya matumizi salama ya gesi ya kupikia kwa wananchi kupitia mtandao wa vijana wa Skauti nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho na utiaji saini wa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas, Benoit Araman alisema kitabu hicho ni nyenzo muhimu ya kujifunzia na kufundishia matumizi sahihi ya gesi ya LPG, huku ushirikiano na Skauti ukilenga kuhakikisha elimu hiyo inawafikia Watanzania wengi zaidi.
Alisema pamoja na kuwa kampuni ina wajibu kwa wanahisa, wafanyakazi na Serikali, inaamini wananchi ndio wadau wake wakuu, hivyo imeamua kuwekeza katika elimu ya usalama ili kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya gesi.
"Tunataka kuona Watanzania wengi zaidi wakitumia gesi ya LPG kwa usalama. Hatuwezi kuwafikia mamilioni ya watumiaji peke yetu, ndiyo maana tumeamua kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania ambacho kina mtandao mkubwa wa vijana wanaoweza kuifikisha elimu hii kwa jamii," alisema.
Alieleza kuwa kupitia makubaliano hayo, Oryx Gas itawajengea uwezo wakufunzi wa Skauti ambao baadaye watawafundisha wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia mbinu ya kumfundisha mkufunzi ili naye awafundishe wengine.
Araman alisema kitabu hicho kimeandaliwa kwa ushirikiano na Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas, Peter Ndomba, kikilenga kuwa rejea ya kudumu kwa watumiaji wa gesi ya LPG, licha ya dunia kuendelea kutumia zaidi mifumo ya kidijitali.
"Ni muhimu kuwa na nyenzo ambayo mtu anaweza kuishika mkononi, akaisoma mara kwa mara na kuirejea kila anapohitaji kujifunza matumizi salama ya gesi," alisema.
Alitangaza rasmi uzinduzi wa kitabu hicho, akisema kitapatikana katika nakala za kuchapishwa pamoja na mfumo wa kidijitali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.
Kwa upande wake, Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas na mtunzi wa kitabu hicho, Peter Ndomba, alisema wazo la kuandika kitabu lilitokana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni baada ya kuona kuwa pamoja na kampeni za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, elimu ya usalama ni muhimu kwa kila mtumiaji.
"Tunahakikisha kila anayechagua kutumia bidhaa yetu ya gesi anakuwa salama. Kitabu hiki kitampa mtumiaji uelewa mpana wa matumizi salama ya gesi ya LPG na kitatumika pia kufundishia katika taasisi mbalimbali ikiwemo shule mara baada ya kukamilisha taratibu za kupata hatimiliki," alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchatta, alisema tukio hilo si la kusaini makubaliano pekee, bali ni mwanzo wa safari ya kuwajengea vijana maarifa, ujuzi na fursa zitakazochangia maendeleo ya taifa.
Alisema Skauti inaamini kuwa kijana mwenye maarifa, maadili na nidhamu ni nguvu muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, hivyo ushirikiano huo utasaidia kuwajengea vijana uwezo katika matumizi ya nishati safi, ajira na usalama.
"Tutahakikisha ushirikiano huu unatekelezwa kwa umakini ili vijana wetu wawe mabalozi wa elimu ya matumizi salama ya gesi na kusaidia kupunguza ajali zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya LPG," alisema.
Naye Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Abubakar Mtitu, alisema ushirikiano huo unaendana na misingi ya Skauti ya kuitumikia jamii na kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Alisema Skauti itaendelea kutumia mtandao wake wa vijana kueneza elimu ya matumizi salama ya gesi pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kuchangia ustawi wa jamii na mazingira.












No comments:
Post a Comment