Na. Mwandishi Wetu - Arusha
Tanzania ipo tayari kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) ikiwa mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda ambapo maandalizi yamefikia hatua nzuri kwa kuzingatia viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) vinavyotakiwa.
Akizungumza hii leo Julai 3, 2026 Jijini Arusha kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ya Maandalizi ya Michuano hiyo, Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha michuano hiyo inafana kwa kuzingatia mipango na mikakati thabiti iliyopo.
Dkt. Abbasi ameiongoza Kamati hiyo iliyotembelea viwanja vitakavyotumika wakati wa michuano hiyo ikiwemo Kiwanja cha Mazoezi cha Mgambo, kiwanja cha mazoezi cha Engutoto, Kiwanja cha mazoezi Magereza, uwanja Mpya wa Arusha pamoja na ukaguzi wa barabara za mjini zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania-TANROADS pamoja na zinasosimamiwa na Wakala wa Barabara za mjini na vijijni -TARURA zitakazoingia na Kutoka Katika uwanja wa Arusha, kujionea maendeleo ya ukarabati na maboresho mbalimbali kuelekea michuano hiyo.
Aidha amesema kuwa, michuano hiyo itakuwa ya kihistoria kwa kukutanisha na kuvutia mamilioni ya watu barani Afrika na duniani kote, ambapo ni kwa mara ya kwanza mashindano hayo kuandaliwa kwa pamoja na Mataifa matatu ya Afrika Mashariki.
"Ni wakati wetu sasa, kuipa nchi heshima yake kuelekea Michuano hiyo ya AFCON, kila mmoja akae tayari katika eneo lake na kujua kuwa anajukumu la kuifanikisha michuano hii na kwa viwango vya kimataifa," alisema Dkt. Abbasi.
Pia alisisistiza Wakandarasi kwenye miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu kuongeza kasi ili kumaliza kazi hizo kwa wakati bila kukwambisha maandalizi hayo.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Nguvila amesema kuwa mkoa umeendelea na maandalizi yote muhimu ikiwemo ya ukarabati wa miundombinu itakayotumika, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji, kuboresha maeneo ya utoaji wa huduma za kiafya ikiwemo hospitali, masuala ya mawasiliano, pamoja na umeme na kuhakikisha vinapatikana kwa ubora na viwango.









No comments:
Post a Comment