"TANZANIA, MALAWI KUHARAKISHA MRADI WA UMEME WA MEGAWATI 180.2 – PROF. SHEMDOE AONGOZA KIKAO." - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, July 11, 2026

"TANZANIA, MALAWI KUHARAKISHA MRADI WA UMEME WA MEGAWATI 180.2 – PROF. SHEMDOE AONGOZA KIKAO."


Na OWM–TAMISEMI, Lilongwe, Malawi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe (SONGWECOM) kilichofanyika Julai 10, 2026 jijini Lilongwe, Malawi, kwa lengo la kujadili kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Maendeleo wa Bonde la Mto Songwe.

Mradi huo unatarajiwa kujengwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi na kuzalisha umeme wa megawati 180.2, huku ukiwa na manufaa makubwa katika sekta za umwagiliaji, usambazaji wa maji, uvuvi, utalii pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa nchi hizo mbili.


Kikao hicho kilijadili hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi, ikiwemo kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati, kwa manufaa ya wananchi wa pande zote za Bonde la Mto Songwe.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Kasper Kasper Mmuya, na wataalamu mbalimbali kutoka Serikali za Tanzania na Malawi.

Baraza la Mawaziri la Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe (The Joint Songwe River Basin Commission – SONGWECOM) linaundwa na Mawaziri kumi kutoka Tanzania na Malawi wanaowakilisha sekta tano muhimu ambazo ni Maji, Nishati, Kilimo cha Umwagiliaji, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Ardhi, ndilo chombo cha juu cha maamuzi kinachosimamia shughuli za Kamisheni hiyo.

Kupitia kikao hicho, Tanzania na Malawi zimeendelea kudhihirisha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika usimamizi endelevu wa rasilimali za Bonde la Mto Songwe, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati, kuimarisha usalama wa maji na chakula, na kuchochea maendeleo endelevu ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

No comments:

Post a Comment