(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF-London)
Tanzania imeandika historia mpya katika masoko ya fedha ya kimataifa baada ya hatifungani ya kwanza inayotolewa nje ya nchi (Tanzania off-shore Bond) yenye thamani ya dola za Marekani milioni 100, sawa na takriban shilingi bilioni 262.5 za Tanzania, iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa, mwanachama wa Kundi la Benki ya Dunia (IFC) kwa kutumia sarafu ya Tanzania, kuorodheshwa katika Soko la Hisa la London, Uingereza.
Fedha hizo zimeekezwa Benki ya NMB Plc kwa njia ya mkopo, ambako zitatumika kuwaendeleza kimtaji wafanyabiashara wadogo na wa kati (MSMEs), huku asilimia 20 ya fedha hizo sawa na takriban shilingi bilioni 52.5 zimetengwa kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wanawake.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, baada ya kupiga kengele kuashiria uzinduzi wa hati fungani hiyo na kufunga biashara ya soko la hisa kwa siku hiyo, Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alisema mafanikio hayo yanafungua ukurasa mpya wa kuiwezesha Tanzania kujenga imani zaidi kwa wawekezaji wa kimataifa na kupanua vyanzo vya mitaji kwa ajili ya Dira 2050.
“Huu ni mwanzo wa hatua muhimu katika safari ya Tanzania ya kushiriki kikamilifu katika masoko ya mitaji ya kimataifa kwa kutumia sarafu yetu wenyewe. Uorodheshwaji huu unaonesha imani kubwa ya taasisi za kifedha za kimataifa kwa uchumi wetu na mwelekeo wa mageuzi ya sekta ya fedha nchini,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Aidha, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa uorodheshwaji wa hatifungani hiyo katika soko kubwa na lenye hadhi duniani kama London Stock Exchange, unaipa Tanzania thamani ya kipekee ya sifa na ishara chanya kwa wawekezaji, jambo litakalosaidia kuboresha uwezo wa nchi kukopa na kukopesheka kwa gharama nafuu.
“Lengo letu si tu kuona dhamana hii inafanikiwa katika soko la kimataifa, bali pia kuhakikisha kuwa matokeo yake yanaonekana moja kwa moja katika ukuaji wa sekta binafsi, hususan kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao ni nguzo muhimu ya uchumi wetu,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Naye Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alieleza furaha yake kuhusu hatua hiyo na kwamba fedha zilizopatikana zitasaidia kuchachua uchumi wa nchi kwa kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati, jambo litakaloongeza kasi ya ukuaji wa sekta binafsi, ajira na shughuli za uzalishaji nchini.
“Hii ni mara ya pili kwa benki yetu kunufaika na Soko la Hisa la London ambapo mwaka 2023 tulipata zaidi ya shilingi bilioni 400 kupitia Hati Fungani ya Jamii na sasa tumepata zaidi ya shilingi bilioni 262.5 kupitia hati Fungani ambayo kwa mara ya kwanza imeorodheshwa kwa sarafu ya Tanzania” Alisema Bi. Zaipuna.
Kwa Upande wake, makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia masuala ya Hazina, Bw. Jorge Familiar, alisema kuwa Benki ya Dunia inajisikia fahari kushirikiana na Tanzania kutimiza malengo yak ya kukuza uchumi wake jumuishi kupitia utekelezaji wa Dira ya taifa ya Maendeleo 2050.
“Tunacho kiangalia sisi si tu kiwango cha fedha tunachowekeza kwa kushrikiana na washirika wetu bali ni matokeo ya uwekezaji huu ambapo tunaamini fedha hizi zitaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii na tunakadiria kuwa zaidi ya watu elfu 13 hadi 20 wakiwemo wanawake watapata ajira na wakati huo huo wawekezaji wa kimataifa wamepata nafasi ya kuwafikia wafanyabiashara kwa kuwekeza” alisisitiza Bw. Familiar.
Kwa ujumla, uorodheshwaji wa hatifungani hiyo unatajwa kuwa ni hatua ya kimkakati inayoiweka Tanzania katika nafasi bora zaidi ya kushindana katika soko la kimataifa la fedha, huku ukiunga mkono jitihada za kukuza uchumi jumuishi na endelevu.
Benki ya Dunia kupitia Taasisi yake ya IFC, imewekeza nchini Tanzania zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.6 ambazo zimekezwa katika miradi mbalimbali ya kimkakati inayokwenda sambamba na malengo ya serikali kuitia seka binafsi katika miradi ya miundombinu, kilimo, masoko ya mitaji na nishati.





No comments:
Post a Comment