TANZANIA YANUNUA NA KUIFADHI DHAHABU TANI 28 MIEZI 18 ILIYOPITA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 7, 2026

TANZANIA YANUNUA NA KUIFADHI DHAHABU TANI 28 MIEZI 18 ILIYOPITA


Na Benny Mwaipaja, Banjul, Gambia


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kwamba katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, Benki Kuu ya Tanzania imenunua na kuhifadhi takriban tani 28 za dhahabu, zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.68 (thamani ya dhahabu iliyopo kwa bei ya jana), sawa na shilingi trilioni 9.76, ikiwa ni Mkakati wa Serikali wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, thamani ya shilingi, uthabiti wa sekta ya fedha na ukuaji wa uchumi.

Bw. Tutuba aliyasema hayo wakati akishiriki mjadala kuhusu Mikakati ya Ununuzi wa Dhahabu ya Benki Kuu (Central Bank Gold Operations), ikiwa ni sehemu ya mijadala ya Mkutano wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), African Caucus 2026, unaozihusisha nchi 54 za Afrika, unaofanyika Banjul nchini Gambia.

Alisema kuwa mpango huo wa kununua dhahabu si tu kwamba umeiwezesha nchi kuhifadhi dhahabu kama mbadala wa kutunza fedha za kigeni, lakini pia umeongeza urasimishaji kwenye sekta ya madini na ujumuishi wa kifedha kwa wauza madini hayo, wakiwemo wachimbaji wadogo, ambapo Benki Kuu imewezesha makundi hayo kufungua zaidi ya akaunti 4,000 katika taasisi mbalimbali za fedha hususan benki.

Gavana Tutuba alieleza kuwa kutokana na bei nzuri ya soko ambayo Benki Kuu inatoa kwa wafanyabiashara wa madini, kumekuwa na mwitikio chanya wa wafanyabuashara na wachimbaji kuiuzia dhahabu Benki Kuu ya Tanzania.

“Tunawalipa wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kwa wakati, ndani ya saa 24 tangu kufanyika kwa mauzo, na tunawalipa kwa bei ya soko la dhahabu la London ya siku hiyo, hatua inayowavutia kuiuzia dhahabu Benki Kuu." Alisema Gavana Tutuba.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongizwa na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na umewashirikisha pia Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria anaye hudumia pia shughuli za kibalozi katika
nchi ya Gambia, Mhe. Balozi Selestine Kakele.

Mkutano huo umewakutanisha wadau wakiwemo viongozi wa Afrika, watunga sera, wataalamu wa fedha, washirika wa maendeleo, kutoka nchi 54 za Bara la Afrika pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Mkutano huo wa African Caucus, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha SDJK, jijini Banjul, ni jukwaa linalowakutanisha magavana wa Afrika katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia, ambalo huzisaidia nchi za Afrika kuzungumza kwa sauti moja kuhusu masuala kama usimamizi wa madeni, fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya miundombinu, kupunguza umasikini, kukuza ajira, biashara, na mageuzi ya kiuchumi


No comments:

Post a Comment