Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Bw. Deogratius Kwiyukwa, amesema kuwa uunganishaji nguvu ya pamoja ya Taasisi za kifedha katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, utachochea ujenzi wa viwanda vitakavyokuwa chachu ya kukuza maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kiuchumi na kijamii.
Bw. Kwiyukwa, amesema hayo kando ya Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week) unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (ICC), jijini Durban, nchini Afrika Kusini.
Alisema kuwa TIB ambayo ni Taasisi ya Serikali imeshiriki katika mkutano huo kutafuta fursa za kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha ndani ya ukanda wa SADC ili kuunganisha mitaji kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo itakayo changia kufikia lengo la utekelezaji wa DIRA ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotaka uchumi wa Tanzania ufikie thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka huo.
Bw. Kwiyukwa alisisitiza kuwa ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa za kilimo, madini adimu, na bidhaa nyingine vitakavyochochea ajira na mauzo ya nje unahitaji uwekezaji mkubwa wa mitaji.
Alisema kuwa Tanzania imewekeza kwenye reli ya SGR, bandari, nishati, barabara na usafirishaji, hatua inayofuata ni kuhakikisha mali hizo zinazalisha shughuli za kiviwanda kuunganisha SGR, bandari, umeme na hifadhi za viwanda, kanda maalum za kiuchumi, maeneo ya madini, vituo vya kilimo na masoko ya nje.
Alisema kuwa TIB, kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Fedha za Ukanda wa SADC, inaweza kufadhili mifumo mizima ya kiuchumi inayozunguka miundombinu hiyo ya reli inayochochea viwanda kando ya njia yake, bandari inayosaidia biashara ya ghala na usafirishaji, umeme wa uhakika unaovutia viwanda vinavyotumia nishati nyingi.
Alisema kuwa mpaka sasa TIB imeviwezesha viwanda na sekta nyingine kadhaa za umma kupata mikopo nafuu kwa ajili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kama vile kahawa, sukari, miradi ya maji na kwamba ikiwezeshwa zaidi kimtaji itafanya mambo makubwa zaidi.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo wamebainishwa kuwa wamevutiwa na fursa nyingi zinazopatikana nchini Tanzania na kuahidi kutafuta taarifa zaidi za maeneo wanayotaka kuwekeza.
Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda wa SADC umewakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za kifedha, wataalamu na wadau wa maendeleo kutoka nchi wanachama wa SADC na unafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kukuza Viwanda Imara, Endelevu na Jumuishi kupitia Maendeleo ya Miundombinu, Mageuzi ya Kilimo na Madini kwa Ajili ya Dunia Yenye Haki.”
Kwa ujumla, mijadala ya Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC jijini Durban imeweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza thamani ya rasilimali za madini na bidhaa nyingine kabla ya kuuzwa nje, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda, miundombinu na miradi ya maendeleo.








No comments:
Post a Comment