UTAFITI WAFICHUA UKATILI WA KIJINSIA, ATHARI ZA TABIANCHI KATIKA SEKTA YA UVUVI MDOGO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, July 9, 2026

UTAFITI WAFICHUA UKATILI WA KIJINSIA, ATHARI ZA TABIANCHI KATIKA SEKTA YA UVUVI MDOGO



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, athari za mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya matumizi ya maeneo ya pwani vimetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoathiri sekta ya uvuvi mdogo nchini, huku wadau wakitaka hatua za haraka kulinda haki za wavuvi na kuhakikisha rasilimali za bahari zinatumika kwa njia endelevu.

Hayo yamebainishwa kupitia matokeo ya utafiti wa mradi wa Sustainable Oceans ulioanza mwaka 2024 na kufanywa kwa ushirikiano kati ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Taasisi ya Kidenmaki ya Haki za Binadamu (DIHR), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, FAO, GIZ, TAFIRI na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Akizungumza matokeo ya utafiti huo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Patience Ntwina, alisema wanawake wanaojishughulisha na ukusanyaji, uchakataji na biashara ya samaki ndio wanaoathirika zaidi na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwemo kuombwa rushwa ya ngono ili waweze kupata samaki.

Alisema utafiti uliofanyika katika mikoa yote ya mwambao wa Bahari ya Hindi, ikiwemo Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara, pia umebaini kuwa miundombinu duni ya maeneo ya kutua samaki hulazimu wanawake kuingia majini kupokea samaki kutokana na boti kushindwa kufika nchi kavu, hali inayowaweka katika mazingira yanayochochea vitendo vya unyanyasaji.

"Changamoto nyingine ni waathirika wengi kushindwa kutoa taarifa kwa mamlaka kwa hofu ya kunyimwa fursa za kufanya biashara au kufanyiwa vitendo vya kulipiziwa kisasi wanaporejea katika maeneo yao ya kazi," alisema Ntwina.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga, alisema bado wanawake wanakabiliwa na vikwazo vya kushiriki kikamilifu katika sekta ya uvuvi kutokana na mifumo ya usimamizi ambayo haijatoa fursa sawa kwa jinsia zote.

Alisema baadhi ya wanawake hawaonekani kama wanastahili kuwa wavuvi au kumiliki vyombo vya uvuvi, hivyo akasisitiza umuhimu wa kutekeleza sheria na sera zinazolinda usawa wa kijinsia na kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa ya kumiliki rasilimali na kushiriki katika maamuzi ya sekta hiyo.

Naye Merina Julius, msimamizi wa wavuvi wadogo kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Fukwe (BMU) Wilaya ya Pangani, alisema athari za mabadiliko ya tabianchi zimechangia kupungua kwa samaki, jambo linaloongeza ushindani wa rasilimali na kuwaweka wanawake katika mazingira hatarishi zaidi ya kukumbana na ukatili wa kijinsia.

Aliongeza kuwa sekta hiyo pia inakabiliwa na migogoro ya matumizi ya maeneo ya bahari, ambapo boti za wavuvi hupita katika mashamba ya mwani na kuharibu mazao, hali inayozua migogoro kati ya wavuvi na wakulima wa mwani ambao wengi wao ni wanawake.

Kutokana na changamoto hizo, wadau wa utafiti wamependekeza kuimarishwa kwa usimamizi wa maeneo ya uvuvi kwa kuweka mipaka ya wazi kati ya maeneo ya uvuvi na kilimo cha mwani, kudhibiti matumizi ya zana haramu za uvuvi, kufunga baadhi ya maeneo ya uvuvi kwa muda ili kuruhusu samaki kuzaliana, pamoja na kuhakikisha wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika maamuzi na uongozi wa sekta ya uvuvi.

Wamesema utekelezaji wa mapendekezo hayo utasaidia kulinda haki za binadamu, kuimarisha usawa wa kijinsia na kuhakikisha sekta ya uvuvi inaendelea kuchangia ajira, usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi wa jamii za mwambao.




No comments:

Post a Comment