NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imezitaka taasisi za maendeleo, sekta binafsi na wananchi wenye uwezo kujitokeza kuchangia Mfuko wa Taifa wa Elimu ili kuongeza rasilimali zitakazowezesha kuboresha miundombinu ya elimu na kuimarisha uwekezaji katika elimu ya amali nchini.
Akizungumza leo Julai 11, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mjumbe wa Bodi ya TEA, Godfrey Boniventura, amesema jukumu la kutoa elimu bora nchini si la Serikali pekee, bali linahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali kupitia michango katika Mfuko wa Taifa wa Elimu unaosimamiwa na TEA kwa mujibu wa sheria.
Amesema TEA ina jukumu la kutafuta rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo, sekta binafsi na watu binafsi ili kuongeza fedha za kuwekeza katika miradi ya maendeleo ya elimu, hususan uboreshaji wa miundombinu na programu zinazolenga kuongeza ujuzi kwa wanafunzi.
Boniventura amesema juhudi hizo zinaendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Elimu 2050, ambayo inaweka mkazo katika kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na uzalishaji.
Ameeleza kuwa TEA inaipa kipaumbele elimu ya amali ili kuhakikisha kila mwanafunzi anayehitimu ngazi yoyote ya elimu anakuwa na ujuzi wa kujitegemea, kujiajiri au kuanzisha shughuli za uzalishaji zitakazochangia kukuza uchumi wa taifa.
"Malengo yetu ni kuona tunapata vijana wenye ujuzi wa kutosha, ambao siyo tu watajiajiri bali pia wataweza kuajiri wengine na kuwa sehemu ya nguvu kazi inayochochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania," amesema.
Ameongeza kuwa Bodi ya TEA kwa kushirikiana na menejimenti itaendelea kutafuta rasilimali nyingi zaidi na kuhakikisha fedha zinazopatikana kupitia Mfuko wa Taifa wa Elimu zinaelekezwa katika miradi yenye tija, hususan inayokuza elimu ya amali na maendeleo ya ujuzi.
Aidha, ametoa rai kwa washirika wa maendeleo, makampuni binafsi na wananchi wenye uwezo kutumia fursa ya kuchangia mfuko huo, akisema michango yao itakuwa uwekezaji wa moja kwa moja katika maendeleo ya taifa kupitia elimu.
Amesema pamoja na kuchangia maendeleo ya elimu, wadau wanaochangia mfuko huo hutambuliwa na mamlaka kwa mchango wao katika kujenga taifa lenye rasilimali watu wenye ujuzi na uwezo wa kuzalisha.
Boniventura pia ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuipa TEA ushirikiano na msaada katika utekelezaji wa majukumu yake, huku akiiomba kuendelea kushirikiana na mamlaka katika kuhamasisha wadau wengi zaidi kushiriki kuchangia Mfuko wa Taifa wa Elimu.
"Ni muhimu Watanzania wote watambue kuwa kuboresha elimu na kuandaa kizazi chenye ujuzi si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mdau anayeguswa na maendeleo ya taifa," amesema.

No comments:
Post a Comment