WAFANYAKAZI TIANPIN WAMLILIA DC NKINDA, WADAI MAZINGIRA HATARISHI YA KAZI NA KUKOSA HAKI ZA MSINGI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, July 15, 2026

WAFANYAKAZI TIANPIN WAMLILIA DC NKINDA, WADAI MAZINGIRA HATARISHI YA KAZI NA KUKOSA HAKI ZA MSINGI


Mkuu wa Wilaya ya Kahama Frank Nkinda aliyevaa shati jekundu lenye madoa meupe akiwa na kamati ya usalama ya wilaya baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya TIANPIN pamoja na Msimamizi mkuu wa mgodi huo Chen Faping ambaye ni raia wa China (kulia) aliyevaa shati la kaki


Na Neema Nkumbi, Kahama


Wafanyakazi wa kampuni ya Tianpin Investment Management Ltd wilayani Kahama wameiomba Serikali kuingilia kati changamoto wanazodai kukabiliana nazo katika eneo lao la kazi, ikiwemo ukosefu wa mikataba ya ajira, mazingira yasiyo salama, kutopatiwa vifaa kinga (PPE) pamoja na hofu ya kutoa malalamiko kutokana na kuogopa kupoteza ajira zao.

Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, wafanyakazi hao wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikihatarisha usalama wao na afya zao wanapotekeleza majukumu katika shughuli za uchimbaji.

Mfanyakazi wa kampuni hiyo, Amos Daudi, amesema wafanyakazi wengi wamekuwa wakifanya kazi bila mikataba rasmi ya ajira, hali inayowafanya kuishi kwa hofu na kushindwa kufikisha malalamiko yao kwa uhuru.

"Watu wengi hapa hawana mikataba ya ajira, Wanaogopa kusema kwa sababu wanaogopa kufukuzwa kazi, Mimi nimeamua kusema kwa niaba ya wenzangu kwa sababu siogopi kufukuzwa kazi nilizaliwa mara moja na nitakufa mara moja," amesema Daudi.

Daudi pia amedai kuwa mazingira ya kazi katika maeneo ya mgodi si salama, akieleza kuwa kuna changamoto ya maji yanayotokana na shughuli za uchimbaji pamoja na maji machafu yanayodaiwa kuelekezwa kwenye maeneo yanayotumiwa na wananchi.

"Yale maji yanayotoka chini kwenye maduara yanashuka mpaka kwenye makazi ya watu pia yanachanganyika na maji machafu yanayotoka kwenye shimo la choo. Pia maji yanatumika hapa kambini kwa kuandaa chakula na kuoga Kwa kweli si salama," amesema.

Akizungumzia suala la usalama kazini, Daudi amedai kuwa baadhi ya wafanyakazi hawapati vifaa muhimu vya kujikinga licha ya kufanya kazi katika maeneo yenye hatari.

Mfanyakazi mwingine, Ngolo Mgema, ameeleza changamoto zinazowakabili wafanyakazi wanaotumia kemikali katika shughuli zao, akidai kuwa baadhi yao wamekuwa wakipata madhara ya kiafya kutokana na mazingira wanayofanyia kazi.

"Tunatumia kemikali mbalimbali ambazo ni hatari kwa afya ya mtu, hasa katika maswali ya afya uzazi kwenye macho, wengine wanawasha uso na ngozi, lakini vifaa vya kujikinga havitoshelezi," amesema Mgema.

Meneja wa Mgodi wa Tianpin Investment Management Ltd amekiri kuwepo kwa changamoto hususan kwenye eneo la usalama na utoaji wa vifaa kinga kwa wafanyakazi.

"Kuhusu masuala ya safety tumekuwa tukipaza sauti sana, Tumewaeleza viongozi wa kampuni, lakini bado kuna changamoto ya wafanyakazi kupata vifaa wanavyostahili," amesema meneja huyo.

Msimamizi mkuu wa mgodi huo Chen Faping amekanusha kuwepo kwa changamoto zilizolalamikiwa na wafanyakazi hao, akieleza kuwa vifaa kinga vipo na wanapewa, na mavazi ameagiza kutoka China baada ya siku 14 yatafika.

“Hakuna hiyo changamoto, vifaa kinga vipo stoo, mavazi tumeagiza baada ya siku 14 yatafika hapa. Naahidi.”

Afisa Madini Mkazi wa Kahama, Mhandisi Chone Malembo, amesema kwa mujibu wa sheria, meneja wa mgodi ndiye mwenye wajibu wa kuhakikisha shughuli zote za mgodi zinaendeshwa kwa kuzingatia taratibu za usalama, afya na mazingira.

"Shughuli zote za mgodi zinasimamiwa na meneja wa mgodi kwa mujibu wa sheria hata kama kuna watu wengine wanaotekeleza majukumu, wanatekeleza kwa niaba ya meneja ambaye ndiye mwenye majibu ya mwisho," amesema Malembo.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi na ukaguzi wa haraka ili kubaini ukweli wa madai yaliyotolewa na kuhakikisha sheria zinafuatwa.

"Tutakwenda kukagua kama safety boots zipo na Kama hazipo kwa ajili ya wafanyakazi hawa, tutaelekeza wasifanye kazi kwenye mazingira hatarishi mpaka mtakapohakikisha mmewapatia vifaa wanavyotakiwa kuwa navyo," amesema Nkinda.

Dc Nkinda amesema Serikali ya awamu ya sita imelenga kuleta tabasamu kwa wananchi wake hivyo itaendelea kusimamia usalama wa wafanyakazi na kuhakikisha waajiri wanazingatia sheria za kazi pamoja na kanuni za usalama migodini.

No comments:

Post a Comment