WAKULIMA WALIPWA SH. TRILIONI 2.3 KUPITIA STAKABADHI ZA GHALA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 31, 2026

WAKULIMA WALIPWA SH. TRILIONI 2.3 KUPITIA STAKABADHI ZA GHALA



Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA


Wakulima na wazalishaji wa mazao nchini wameendelea kunufaika na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS), baada ya kulipwa zaidi ya Sh trilioni 2.298 katika mwaka wa fedha 2025/26, huku kiasi cha mazao kilichouzwa kupitia mfumo huo kikiongezeka kwa asilimia 43.6, hatua inayoonyesha kuimarika kwa masoko ya mazao na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Bw. Asangye Bangu, amesema hayo leo Julai 31, 2026 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema katika kipindi hicho, jumla ya kilo bilioni 1.122 za mazao tisa ambazo ni korosho, ufuta, kahawa, kakao, mbaazi, dengu, choroko, soya na chai ziliuzwa kupitia minada ya kidijitali inayosimamiwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ikilinganishwa na kilo milioni 781.7 mwaka uliopita, sawa na ongezeko la zaidi ya kilo milioni 340 ndani ya mwaka mmoja.

"Ongezeko hili linaonyesha kuwa wakulima wengi zaidi wameendelea kuuamini Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuamua kuuza mazao yao kupitia utaratibu rasmi wenye ushindani na uwazi," amesema Bw. Bangu.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yameongeza mapato ya Serikali za Mitaa, ambapo zaidi ya Sh bilioni 61.05 zilikusanywa kupitia ushuru wa mazao (CESS), huku thamani ya biashara yote iliyofanyika kupitia mfumo huo ikifikia Sh trilioni 2.679.

Amesema fedha hizo zimechangia kuboresha kipato cha wakulima, kuimarisha ustawi wa kaya na kuziwezesha halmashauri kuboresha huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa barabara, shule, vituo vya afya na miundombinu mingine ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Bw. Bangu, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala umeendelea kukua tangu ulipoanzishwa mwaka 2006 ukiwa unahusisha zao la korosho pekee. Hivi sasa mfumo huo unahusisha mazao na bidhaa 18 na unatekelezwa katika mikoa 23 nchini, hali inayoonyesha kuongezeka kwa imani ya wadau na kupanuka kwa matumizi ya mfumo katika biashara ya mazao.

Amesema kupitia mfumo huo, wakulima huuza mazao yao kwa ushindani kupitia minada rasmi, huyahifadhi katika maghala yenye viwango, hulipwa kupitia benki na taasisi za fedha na wanaweza kutumia stakabadhi za ghala kama dhamana ya kupata mikopo.

Hatua hizo zimechangia kuongeza kipato cha wakulima, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na kuimarisha uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Aidha, amesema mapato ya ndani ya WRRB yameongezeka kutoka Sh bilioni 1.998 mwaka wa fedha 2023/24 hadi Sh bilioni 5.870 mwaka 2025/26.

Vilevile, mfumo huo umezalisha ajira 31,875 kupitia shughuli mbalimbali za ukusanyaji wa mazao, uhifadhi, usafirishaji, upimaji wa ubora na huduma nyingine katika mnyororo wa thamani wa mazao.

Akizungumzia mipango ya mwaka wa fedha 2026/27, Bw. Bangu amesema WRRB imejipanga kupanua Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa kuingiza sekta ya mifugo, ambapo mnada wa kwanza wa mifugo kupitia mfumo huo unatarajiwa kufanyika Wilaya ya Mvomero.

Pia mfumo utapanuliwa kwenye bidhaa nyingine zikiwemo mwani, ngozi na mazao ya bustani, sambamba na kuimarisha matumizi ya TEHAMA, kuongeza ushiriki wa taasisi za fedha na kuhamasisha uwekezaji katika maghala ya kisasa.

Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza fursa za biashara, ajira na uwekezaji, huku zikiunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



No comments:

Post a Comment