WANANCHI LUSHOTO WAMSHUKURU RAIS SAMIA, WAMPONGEZA PROF. SHEMDOE KWA UJENZI WA BARABARA YA MALIBWI - KWEKANGA-NGWELO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 17, 2026

WANANCHI LUSHOTO WAMSHUKURU RAIS SAMIA, WAMPONGEZA PROF. SHEMDOE KWA UJENZI WA BARABARA YA MALIBWI - KWEKANGA-NGWELO


Na Mwandishi wetu, Lushoto


Wananchi wa Jimbo la Lushoto Julai 16, 2026 wamemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa Barabara ya Malibwi–Kwekanga–Ngwelo, wakisema hatua hiyo imeondoa kero ya muda mrefu iliyokuwa ikikwamisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao, na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Lushoto Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, kwa kuifikisha Serikalini changamoto hiyo ambayo imepatiwa ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwekanga, Bw. Salim Khamis Nyongo, amesema barabara hiyo inayojengwa inaunganisha Kata za Malibwi, Kwekanga, Kilole na Ngwelo pamoja na Jimbo la Mlalo, hivyo ni mhimili muhimu wa uchumi kwa wananchi wa eneo hilo ambao ni wakulima wa nyanya, viazi na karoti.

“Kwa miaka mingi tumeshindwa kusafirisha mazao yetu kwa urahisi kutokana na ubovu wa barabara, hivyo tunamshukuru Rais Samia kwa kututatulia kero yetu ya barabara na tunampongeza Prof. Shemdoe kwa kuwasilisha kero yetu na hatimaye imetatuliwa,” amesema Bw. Nyongo.

Bi. Rukia Selemani, Mkazi wa Kijiji cha Kwekanga amesema kuwa kabla ya kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kusafirisha mazao yao, lakini hata wakati ujenzi ukiendelea tayari wameanza kuona manufaa yake kwani imewarejeshea matumaini na kuwaletea tabasamu, hivyo wanamshukuru Prof. Shemdoe kwa kuhakikisha changamoto hiyo inafanyiwa kazi. 

Kwa upande wake, Bi. Fadhila Salehe ambaye pia ni mkazi wa kijiji cha Kwekanga amesema hapo awali magari yalikuwa yakiishia Malibwi, jambo lililowalazimu wananchi kubeba mizigo kichwani au kutumia pikipiki kwa gharama kubwa, hivyo amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara hiyo na kumpongeza Mhe. Prof. Riziki Shemdoe kwa ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa mradi huo.

Naye Bi. Biasina Shaban Mtari, Mkazi wa Kijiji cha Kwekanga amesema anashukuru kwa sasa magari kutoka Dar es Salaam, Arusha na Tanga yanafika kwenye makazi ya wananchi pasipo na kikwazo chochote, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Mkazi Mwingine wa Kijiji cha Kwekaga, Bi. Shekela Ramadhan Mohamed amesema ujenzi wa barabara hiyo umeboresha pia maisha ya watoto wanaokwenda shule, kwani zamani walikuwa wakirejea nyumbani wakiwa wamechafuka kutokana na ubovu wa barabara, lakini sasa wanakwenda shuleni na kurejea nyumbani wakiwa wasafi.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Lushoto, Bi. Brand Joseph Nyaki, amesema Barabara ya Malibwi–Kwekanga–Ngwelo inarekebishwa kwa kiwango cha zege na Mkandarasi Ms. Broader Construction Company Ltd, ikihusisha tabaka la zege lenye unene wa milimita 150 kwa urefu wa kilomita 1.5.

Bi. Nyaki ameongeza kuwa, mradi huo umeleta manufaa ya kiuchumi kwa vikundi vya Songambele, Inuka na Mkombozi vinavyonufaika na miradi ya vikundi kwa huduma wakati wa utekelezaji wa ujenzi huo wa mradi wa barabara, huku akimshukuru Mhe. Prof. Shemdoe kwa kuendelea kusimamia upatikanaji wa miundombinu bora ya barabara inayofungua fursa za maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa Jimbo la Lushoto.

No comments:

Post a Comment