WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba ameendelea kusisitiza suala la amani na usalama nchini na kuwaasa Watanzania watambue kwamba vyama vya siasa siyo sababu ya kuwatofautisha.
“Vyama vya siasa siyo sababu ya kutofautiana kwa sababu sisi wanasiasa tunawasiliana kwa karibu sana na tunasaidiana sana na tena tunakula nyamachoma pamoja. Vyama vya siasa viko, kikatiba na sisi wala hatuna mzozo,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumatano, Julai mosi, 2026) wakati akizungumza na mamia ya wananchi kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Sokoine, vilivyopo Mugumu, wilayani Serengeti, mkoani Mara.
“Watanzania wenzangu, Serikali ikiwaambia jambo mjue kuwa tuna taarifa za kutosha. Msiruhusu kugombanishwa na mada nyepesi nyepesi. Ninawasihi Watanzania tukatae kushirikiana na watu wasioitakia mema nchi yetu,” amesisitiza na kuongeza: "Huu uhalifu siyo dhidi ya Rais wala vyama vya siasa bali ni dhidi ya usalama wa nchi yetu. Watanzania tuwe mstari wa mbele kulinda usalama wa nchi yetu."
“Amani ikivurugwa, muathirika wa kwanza ni mwananchi mwenyewe. Kila Mtanzania ni mlinzi wa nchi yake. Kila Mtanzania afumbue macho, tuamke, tukatae matendo yao ya kutaka kutumia damu za Watanzania ilhali wao wanalipwa mamilioni ya fedha,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye ameanza ziara ya siku tano mkoani Mara, anatarajiwa kutembelea wilaya zote sita na halmashauri zote tisa ambapo atakagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya sh. bilioni 52. 9 na kuzungumza na wananchi.
Mapema, Dkt. Mwigulu alikagua mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambao unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 4.5 hadi kukamilika kwake.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Msanifu Majengo wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Mara, Bw. Nicholas Jeje, alisema mradi huo ambao ujenzi umefikia asilimia 42, ulianza Aprili 10, 2025 na unatarajiwa kukamilika Aprili, 2028.
“Pindi litakapokamilika, jengo hilo litakuwa na ofisi 62, zikiwemo ofisi za Mkurugenzi wa Halmashauri na Mwenyekiti wa Halmashauri, pamoja na kumbi mbili za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 50 na 110 mtawalia, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema.






No comments:
Post a Comment