AfDB YAANZA UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA MRADI WA BWAWA LA FARKWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 27, 2026

AfDB YAANZA UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA MRADI WA BWAWA LA FARKWA


Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeanza ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Farkwa mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuhakikisha miradi ya kimkakati ya Sekta ya Maji inatekelezwa kwa ufanisi.

Ujumbe wa AfDB unaoongozwa na Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Benki hiyo, Bw. Mitchera Chirwa, umefika nchini na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kuhusu maendeleo ya Sekta ya Maji pamoja na fursa za uwekezaji.

Katika mazungumzo hayo, AfDB imesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza na kufadhili miradi ya kimkakati ya Sekta ya Maji, ikiwemo Mradi wa Bwawa la Farkwa.

Mhandisi Waziri ameishukuru AfDB kwa mchango wake katika maendeleo ya Sekta ya Maji nchini, akieleza kuwa Mradi wa Bwawa la Farkwa unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza uhaba wa maji katika Jiji la Dodoma.

Aidha, ameiikaribisha AfDB kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati, ikiwemo Gridi ya Taifa ya Maji, inayolenga kusafirisha maji kutoka Mto Rufiji hadi Dar es Salaam, pamoja na mradi wa kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma kupitia Singida.

Pia, Mhandisi Waziri ameomba ushirikiano katika kuboresha huduma za maji katika majiji ya Mwanza, Arusha na Dar es Salaam.

Kwa upande wa maeneo ya vijijini, Mhandisi Waziri ameiomba AfDB kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwafikishia huduma ya maji wananchi wa vijiji 1,575 ambavyo bado havijapata miundombinu rasmi ya huduma ya maji.

Ameongeza kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na AfDB katika uwekezaji, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, pamoja na utekelezaji wa miradi kupitia ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPPs).

Kwa upande wake, Bw. Chirwa amesema maji ni miongoni mwa vipaumbele vya AfDB na kwamba Benki hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ya uhakika na endelevu.

Amesema AfDB imeanza kutoa fursa za ufadhili unaozingatia matokeo (Result Based Financing) na kuitaka Wizara ya Maji kuendelea kuwasilisha maombi ya miradi ya kimkakati kwa ajili ya kuangaliwa na kufadhiliwa.

Sambamba na ziara hiyo, Mkandarasi wa ujenzi wa Bwawa la Farkwa amekamilisha taratibu za awali za mkataba, huku Wizara ya Maji ikitarajia kumkabidhi eneo la ujenzi wa bwawa leo, Agosti 27, 2026.

Ziara ya ujumbe wa AfDB nchini inafanyika kuanzia Agosti 26 hadi 28, 2026, na inahusisha ziara katika Wizara ya Fedha pamoja na kutembelea eneo la ujenzi wa Bwawa la Farkwa lililopo wilayani Chemba, mkoani Dodoma.




No comments:

Post a Comment