DARAJA LA IKINDA LAONDOA KERO YA USAFIRI KWA WANANCHI KAHAMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, August 26, 2026

DARAJA LA IKINDA LAONDOA KERO YA USAFIRI KWA WANANCHI KAHAMA


‎Na Mwandishi Wetu - Kahama, Shinyanga

‎Wananchi wa kata za Ikinda na Bugarama halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameondokana na changamoto ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Ikinda lenye urefu wa mita 11 katika barabara ya Ikinda–Buyange.
‎Daraja hilo limejengwa na TARURA kupitia mradi wa RISE unaotekelezwa kwa fedha za mkopo nafuu toka Benki ya Dunia ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha miundombinu ya barabara na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha usafiri na shughuli za kiuchumi.
‎Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wameeleza kuwa kabla ya ujenzi wa daraja wakati wa msimu wa mvua barabara hiyo ilikuwa ikikatika na kufanya usafiri kuwa mgumu na kuhatarisha usalama wa wananchi na mali zao lakini kukamilika kwa daraja hilo changamoto hiyo sasa imekuwa historia.
‎Kwa upande wake, Meneja wa TARURA wilaya ya Kahama Mhandisi Joseph Mkwizu amesema ujenzi wa daraja hilo umegharimu shilingi milioni 410.02 ambapo mradi umekamilika kwa asilimia 100 kwa sasa upo katika kipindi cha matazamio.
‎Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umejumuisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 11 na upana wa mita 8, kalavati 3, uchongaji wa barabara urefu wa kilomita 4, kunyanyua tuta na kuweka changarawe kilomita 1 pamoja na uwekaji wa alama za barabarani chini ya Mhandisi Mshauri NOR-PLAN Tanzania Ltd huku kazi za ujenzi zikifanywa na M/S Mashilanga Construction Company Ltd.
‎Amesema kuwa zaidi ya kurahisisha usafiri daraja hilo linatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na bidhaa za biashara kwenda kwenye masoko huku wananchi wakipata fursa ya kusafiri kwa uhakika bila hofu ya barabara kukatika wakati wa mvua.
‎Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Mwangonda baada ya kufungua daraja hilo la Ikinda amewataka wananchi kulitunza na kulinda daraja hilo kwa kuepuka kufanya shughuli zozote za kibinadamu pembezoni mwa daraja zinazoweza kuhatarisha uimara wa miundombinu hiyo.
‎Amesema utunzaji wa miundombinu ni jukumu la wananchi na serikali kwa pamoja akisisitiza kuwa kulinda daraja hilo kutasaidia kulifanya lidumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo. Aidha, ametoa pongezi kwa TARURA kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kuhakikisha daraja linajengwa kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika.

No comments:

Post a Comment