Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Uwazi katika usimamizi wa vyama vya ushirika nchini umeongezeka baada ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuunganisha zaidi ya vyama vya ushirika 6,000 katika mfumo wa kidijitali unaowawezesha wakulima kufuatilia mauzo ya mazao yao na malipo wanayostahili kwa wakati.
Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, ameyasema hayo Agosti 2,2026 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Amesema mfumo huo umetengenezwa kwa ushirikiano na Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika kwa lengo la kusimamia shughuli zote za vyama vya ushirika kwa njia ya kidijitali, hivyo kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi.
"Mfumo huu unamwezesha mkulima kufuatilia mazao aliyowasilisha, kujua yameuzwa kwa bei gani na kiasi gani cha fedha anachostahili kulipwa. Hii imeongeza uwazi na kuimarisha imani ndani ya vyama vya ushirika," amesema Kaswaga.
Amesema e-GA ina jukumu la kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika taasisi za umma ili kuhakikisha huduma za serikali zinatolewa kwa ufanisi kupitia mifumo ya kidijitali.
Kaswaga amesema ushiriki wa e-GA katika Maonesho ya Nanenane unalenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo pamoja na mchango wake katika kuharakisha utoaji wa huduma za serikali kwa kutumia teknolojia.
Katika sekta ya kilimo, amesema e-GA imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuendeleza mifumo mbalimbali inayorahisisha ukusanyaji wa taarifa za wakulima, usimamizi wa taasisi na utoaji wa vibali mbalimbali vya kilimo.
Aidha, amesema e-GA imeanzisha kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania mfumo wa Fertilizer Information System (FIS) unaowezesha serikali kufuatilia wazalishaji, waagizaji na wasambazaji wa mbolea pamoja na mwenendo wa soko.
Amesema mfumo huo pia unasaidia kufuatilia utekelezaji wa bei elekezi za mbolea ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa bei stahiki na kuzuia ongezeko holela la bei.
Kaswaga ameongeza kuwa taasisi mbalimbali zinazohudumia sekta ya kilimo zimeendelea kutumia mifumo ya barua pepe za serikali pamoja na mfumo wa e-Office, hatua iliyoongeza ufanisi wa mawasiliano na utendaji kazi serikalini.
"Lengo letu ni kuhakikisha serikali inafanya kazi kwa ufanisi kupitia mifumo ya kidijitali na wananchi wanapata huduma kwa urahisi popote walipo," amesema.
Amesisitiza kuwa e-GA itaendelea kushirikiana na wizara na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanachochea maendeleo ya sekta ya kilimo, ushirika na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.



No comments:
Post a Comment