Wahitimu wa vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini Tanzania wanatarajiwa kuwa na ujuzi unaoendana zaidi na mahitaji ya soko la ajira, kufuatia hatua inayochukuliwa kupitia Mradi wa ESPJII wa kuandaa viwango vya Kazi.
Mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia unalenga kukuza viwango vya ujuzi nchini kwa kuimarisha mifumo ya mafunzo, kuwajengea uwezo walimu pamoja na kuboresha matumizi ya teknolojia katika sekta ya TVET.
Akizungumza kuhusu mchakato huo leo Agosti 27,2026 Mratibu wa Mradi huo Bw. Aggrey Mleli amesema maandalizi ya miongozo ya Viwango vya kazi ni hatua muhimu katika kuhakikisha mafunzo yanayotolewa katika taasisi za TVET yanaendana na mahitaji halisi ya ulimwengu wa kazi.
Mleli amesema kikao cha wadau kilichofanyika ni sehemu ya hatua ya pili ya kupitia na kukusanya maoni kutoka kwa wadau kabla ya miongozo hiyo kupelekwa katika ngazi za juu kwa ajili ya kuidhinishwa na kuanza kutumika katika maandalizi ya kuandaa viwango vya Kazi.
Amesema mchakato huo ni muhimu kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji mapya ya soko la ajira ambayo yameendelea kubadilika, hali inayohitaji mifumo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwenda sambamba na mabadiliko hayo.
“Wahitimu wengi wanapomaliza masomo wanakutana na changamoto ya kutokuwa na ujuzi wa kutosha kutokana na mabadiliko mbalimbali ya teknolojia, kwa hiyo, kupitia mradi huu tunatarajia kuziba hilo pengo,” amesema.
Kwa mujibu wa Mleli, pamoja na uandaaji wa Viwango vya Kazi, ESPJII pia unatekeleza shughuli zinazolenga kuwajengea uwezo walimu, kuboresha mitaala na kuimarisha mifumo ya teknolojia, hatua zinazotarajiwa kuongeza ubora wa mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.
Amesema NACTVET, kama mdhibiti, inaendelea kuhakikisha taasisi nufaika za mradi zinatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya TVET.
Hatua hiyo inatajwa kuwa muhimu katika kujenga mfumo wa mafunzo unaozalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika ajira na uzalishaji, huku vijana wakipewa nafasi kubwa zaidi ya kukabiliana na ushindani wa soko la ajira.
Tanzania ikiendelea kuwekeza katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi, maandalizi ya kuandaa viwango vya kazi yanaonekana kuwa sehemu muhimu ya safari ya kuhakikisha vijana wanaohitimu vyuo hawatoki na cheti pekee, bali wanakuwa na ujuzi unaotambulika na unaohitajika katika ulimwengu halisi wa kazi.







No comments:
Post a Comment