Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa maji Kigamboni kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi pamoja na uwezo wa kuhudumia wananchi ambapo imeshuhudia na kuridhika na uzalishaji wa maji ambao kwa sasa ni Lita milioni 37 kwa siku.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) ametoa uhakika kwa wakazi wa Kigamboni kuhusu upatikanaji wa huduma ya majisafi ambapo kamati imejiridhisha kuwa uzalishaji wa mradi huo unatosheleza mahitaji ya sasa ya Kigamboni ambayo yanafikia Lita milioni 7 kwa siku ikilinganishwa na uzalishaji ambao ni Lita milioni 37 kwa siku.
"Baada ya kuona utekelezaji, Sasa ni muhimu kuwaambia wananchi kutumia fursa hiyo kwa kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa huduma ya maji ili waweze kunufaika na miundombinu iliyowekwa, tayari DAWASA wametoa unafuu wa kuunganishiwa kwa punguzo hivyo ni wakati wa kuchangamkia fursa" Mhe. Kiswaga amesema.
Amesisitiza umuhimu wa DAWASA kushirikiana na wananchi ili huduma inawafikia walengwa wengi zaidi akieleza kuwa uwepo wa uzalishaji wa kutosha unatoa fursa ya kuongeza idadi ya wateja wanaounganishwa katika huduma ya maji.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema Wizara ya Maji kupitia DAWASA imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na kamati na kwamba yatafanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha zaidi huduma ya maji kwa wananchi.
"Kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha huduma ya maji inasogezwa karibu na kila mwananchi na kupatikana kwa uhakika, sambamba na kuendelea kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa maji" Mhe. Aweso amesema.
Ameongeza DAWASA inaendelea na kuchukua hatua za kupunguza kiwango cha maji kinachopotea (NRW) katika mfumo wa uzalishaji na usambazaji, ili kuhakikisha maji yanayozalishwa yanawafikia wananchi wengi zaidi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma hiyo muhimu.










No comments:
Post a Comment