Serikali imekusudia kukomesha uuzaji wa mazao ghafi kwani mfumo huo unamnyima mkulima zaidi ya nusu ya faida halisi na kubainisha kuwa mkakati uliopo ni kuongeza thamani ya mazao kama korosho kabla ya kuyaweka sokoni, hatua itakayoinua kipato cha wajasiriamali na wakulima wadogo mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), wakati wa uzinduzi wa Kiwanda Darasa cha Kubangua Korosho cha Mandiwa Agosti 10, 2026 Wilayani Masasi, Mtwara.
Mradi uliojengwa na Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), ambapo ameeleza kuwa Serikali imeahidi kuendelea kutekeleza miradi inayogusa maisha ya wananchi kwa vitendo kwa kuwekeza kwenye miundombinu na uchumi ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ili wananchi wanufaike moja kwa moja.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali haitaishia kutoa mafunzo kiwandani hapo tu, bali itapanua huduma za kiufundi kwa kusogeza mashine za kubangua korosho na kusindika mazao mengine hadi ngazi za vikundi vya ushirika. Mpango unalenga kusaidia wananchi wa Masasi na Ndanda kupata zana hizo kwa urahisi na kuongeza ufanisi wa uzalishaji katika maeneo yao.
Waziri Kapinga ametoa wito kwa viongozi na jamii kusimamia fedha za miradi kwa uaminifu na kuzuia ubadhirifu, kwa kuwa zinatafutwa kwa jasho la Watanzania.





No comments:
Post a Comment