Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuja na mikakati mipya ya utendaji itakayosaidia kurejesha hadhi ya taasisi hiyo na kuongeza tija na ufanisi kwa Serikali na jamii kwa ujumla.
Akizungumza na Menejimenti ya TEMESA jijini Dodoma leo, Agosti 14, 2026, Balozi, Eng. Amour amesisitiza watumishi wa Wakala huo kufanya kazi kwa weledi, bidii na ubunifu ili kutimiza kikamilifu malengo ya kuanzishwa kwa TEMESA.
“Serikali inaitegemea sana TEMESA katika kutekeleza majukumu iliyokabidhiwa. Hivyo, changamkeni, tunataka kuona tofauti katika muundo, utendaji na maslahi ya watumishi,” amesisitiza Balozi, Eng. Amour.
Aidha, amewataka mameneja wa mikoa kupewa nguvu na mamlaka zaidi ili waweze kuwajibika na kupimwa kwa kuzingatia matokeo ya utendaji katika mikoa wanayoisimamia.
Balozi, Eng. Amour pia amesisitiza umuhimu wa kuondoa migongano ya kimuundo na kiutendaji ndani ya Wakala huo, huku akiwataka viongozi kutekeleza mpango wa mafunzo kwa watumishi ili kuwawezesha wataalamu kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali ni muhimu katika kurahisisha utendaji wa TEMESA, kuongeza ufanisi na kuhakikisha taarifa sahihi zinapatikana kwa wakati zinapohitajika.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Bw. Kheri Mahimbali, amesema Wakala huo umejipanga kuja na taswira mpya ya kiutendaji pamoja na kuboresha muonekano wake, huku akiwataka wadau kuendelea kuwapa ushirikiano ili kufanikisha azma hiyo.
Amesema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha TEMESA inatoa huduma bora kwa haraka, ufanisi na umadhubuti zaidi kwa wananchi na wadau wake.




No comments:
Post a Comment