Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
WATANZANIA wameanza kunufaika na huduma za matibabu ya kibingwa zinazopatikana nchini, hali inayopunguza gharama na ulazima wa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Universal Medical Tourism, Dk. Sharif Mollel, amesema huduma hizo zinapatikana katika Hospitali ya SINO iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam, inayomilikiwa na wawekezaji kutoka China katika sekta ya afya.
Amesema kampuni yake inashirikiana na hospitali hiyo katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibingwa, teknolojia za kisasa za matibabu pamoja na baadhi ya huduma zinazotokana na tiba za jadi za China, zinazojulikana kama Traditional Chinese Medicine.
Dk. Mollel amesema uwepo wa huduma hizo nchini unawapa Watanzania nafasi ya kupata matibabu bila kulazimika kuingia gharama kubwa za tiketi za ndege, malazi, visa na matumizi mengine yanayotokana na safari za matibabu nje ya nchi.
“Lengo letu ni kuona Watanzania wanapata huduma nyingi zaidi hapa nchini. Kama huduma inayohitajika inapatikana Tanzania, hakuna sababu ya mgonjwa kuanza na safari ya kwenda nje ya nchi,” amesema.
Amesema baadhi ya wagonjwa kutoka nchi za Afrika Mashariki na ukanda wa SADC pia wameanza kuja Tanzania kupata huduma katika hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa Dk. Mollel, hatua hiyo inaonesha kuwa Tanzania ina nafasi ya kujijenga kuwa kituo muhimu cha huduma za afya na medical tourism katika ukanda wa Afrika.
“Tunataka kuona medical tourism ikienda pande zote. Siyo Watanzania kwenda nje kutibiwa pekee, bali pia wagonjwa kutoka nchi nyingine kuja Tanzania kupata huduma,” amesema.
Amesema Hospitali ya SINO inatoa huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu kwa kutumia teknolojia za kisasa, sambamba na huduma katika maeneo mbalimbali ya kibingwa.
Miongoni mwa huduma hizo ni matibabu yanayohusiana na mifupa na viungo, mgongo, mfumo wa neva, urology, physiotherapy pamoja na huduma nyingine kulingana na hali na uchunguzi wa mgonjwa.
Hospitali hiyo pia ina teknolojia za uchunguzi zikiwemo Ultrasound, CT Scan na MRI.
Dk. Mollel amesema uwepo wa vifaa na wataalamu hao unasaidia madaktari kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuamua aina ya matibabu yanayomfaa mgonjwa.
Mbali na tiba za kisasa, amesema Hospitali ya SINO inatoa pia baadhi ya huduma zinazotokana na Traditional Chinese Medicine, mfumo wa tiba unaotumika kwa kiwango kikubwa nchini China.
Miongoni mwa huduma hizo ni acupuncture, ambayo hutumia sindano maalumu katika maeneo mahususi ya mwili chini ya usimamizi wa wataalamu.
Amesema huduma hizo zinaweza kutumika kusaidia katika usimamizi wa baadhi ya hali za maumivu, misuli na viungo baada ya mgonjwa kufanyiwa tathmini ya kitaalamu.
Dk. Mollel amesisitiza kuwa huduma za tiba za jadi za China hazikusudii kuchukua nafasi ya tiba za kisasa, bali hutolewa kulingana na ushauri na tathmini ya wataalamu.
Ametoa wito kwa Watanzania, hususan wakazi wa Dar es Salaam, kutumia nafasi ya kuwepo kwa huduma hizo nchini kabla ya kufanya uamuzi wa kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
“Wale wanaohitaji huduma za kibingwa waje wafanyiwe tathmini. Pia, wale wanaopendelea au wanaotaka kufahamu zaidi kuhusu Traditional Chinese Medicine wanaweza kupata huduma hizo hapa Mikocheni,” amesema.
Dk. Mollel amesema moja ya malengo ya Universal Medical Tourism ni kuendelea kuvutia wataalamu, teknolojia na uwekezaji wa afya kutoka nje ya nchi ili huduma nyingi zaidi zipatikane Tanzania.
Amesema kampuni hiyo pia inalenga kuendeleza ushirikiano kati ya madaktari wa Tanzania na wataalamu kutoka China kupitia kambi za matibabu na programu mbalimbali za kubadilishana ujuzi.
“Tunapotengeneza mazingira ya daktari wa Tanzania kufanya kazi pamoja na mtaalamu kutoka China, tunamhudumia mgonjwa lakini pia tunajenga uwezo wa wataalamu wetu,” amesema.
Amesema hatua hiyo inaweza kusaidia teknolojia na maarifa yanayoletwa nchini kubaki na kutumika kwa muda mrefu badala ya huduma kutegemea wataalamu wa nje pekee.
Dk. Mollel amesema dhamira ya muda mrefu ni kuona Tanzania inapunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kusafiri nje kwa huduma zinazoweza kutolewa nchini, huku ikiongeza idadi ya wagonjwa kutoka mataifa mengine wanaokuja kupata matibabu hapa nchini.







No comments:
Post a Comment