Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb.) ameiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kuhakikisha Utekelezaji wa Mipango ya Dharura ya muda mfupi ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi katika Jiji la Dodoma inafanyika kwa haraka ili wananchi, hasa wa maeneo ya Pembezoni wanapata huduma ya maji.
Mhe. Aweso ameagiza pia Mipango hiyo iende sambamba na usimamizi wa karibu kwa kuwa na timu kababe ya kusimamia na kufuatilia Ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Farkwa ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kwa kuwa hakuna kisingizio chochote.
Mhe. Waziri Aweso ametoa maagizo hayo leo Agosti 31 2026 wakati akizungumza na Menejimenti ya Wizara ya Maji na ya DUWASA.
“Timu ijipange vizuri fedha za mradi wa Bwawa la Farkwa zipo hivyo hatuna kisingizio, timu itakayosimamia iwe kabambe na usimamizi wake usiwe wa kawaida ili wananchi wa Jiji la Dodoma wanufaike na kazi kubwa na matunda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan”. Alisema Waziri Aweso
Ameongeza kuwa, kwa sasa Jiji la Dodoma lina mahitaji ya maji lita milioni 159 kwa siku wakati DUWASA kwa sasa inazalisha lita milioni 91 kwa siku, hivyo kufanya upungufu wa maji wa zaidi ya lita milioni 61, ambapo mipango ya muda mfupi na miradi inayotekelezwa inaenda kuongeza uzalishaji wa lita milioni 34 kwa siku.
Mhe. Aweso amewahakikishia wananchi wa Jiji la Dodoma kuwa, Wizara inasimamia kwa nguvu zote kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maji Dodoma inakamilika kwa wakati ili huduma ya maji iwafikie wananchi wote hasa maeneo ya Nkuhungu, Miganga, Mkonze, Chidachi, Michese, Mpamaa na baadhi ya maeneo ya Ihumwa.








No comments:
Post a Comment