Na Shua Ndereka OKULY BLOG, Morogoro
Mkoa wa Morogoro unatarajia kupokea zaidi ya washiriki 6,800 kutoka nchi tano kwa Mashindano ya Michezo ya Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ya nchi wananchama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (Federation of East Africa Schools Sports Association FEASSA) 2026, hatua inayotarajiwa kuufanya mkoa huu kuwa kitovu cha michezo, biashara na utalii kwa siku 12 za mashindano yanayoanza leo Agosti 12 hadi 23, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema mashindano hayo, yatawakutanisha wanafunzi kutoka nchi ya Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania, huku yakifanyika kwa mara ya kwanza katika Mkoa wa Morogoro na kwa mara ya tano nchini Tanzania.
Amesema, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mashindano hayo yamekamilika, huku ikiwakaribisha wananchi na wageni kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kujitokeza kushuhudia mashindano hayo yanayolenga kukuza vipaji vya michezo, kuimarisha mshikamano na urafiki miongoni mwa vijana wa Afrika Mashariki pamoja na kutoa nafasi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kushiriki katika michezo.
Aidha Tanzania itawakilishwa na wanafunzi 1,510 kutoka mikoa yote 26, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kushiriki katika historia ya mashindano ya FEASSA, hatua inayoonesha dhamira ya nchi kuendeleza michezo ya wanafunzi na kuibua vipaji vya vijana.
Malima amesema Mkoa wa Morogoro nao una sababu ya kujivunia baada ya kufuzu kushiriki katika michezo 13 kufuatia mafanikio yaliyopatikana katika mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yaliyofanyika mkoani Iringa, huku akiwataka wanamichezo kushindana kwa nidhamu, uzalendo na kuendelea kuitangaza vyema Tanzania.
Ili kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa mafanikio, viwanja 21 ndani ya Manispaa ya Morogoro vimetengwa kwa ajili ya michezo hiyo, huku maeneo manane yakiandaliwa kwa ajili ya malazi ya washiriki kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, serikali inaendelea kuhakikisha maeneo yote muhimu yanakuwa tayari.
“FEASSA 2026 ni fursa muhimu ya kukuza uchumi wa Morogoro kupitia biashara za malazi, usafiri, chakula na huduma nyingine, sambamba na kuitangaza mkoa huu, kama kitovu cha utalii kwa kuwa wageni watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo Hifadhi za Taifa za Mikumi, Udzungwa na Nyerere pamoja na kujifunza utamaduni wa wananchi wa Morogoro”. Amesema Malima
Pia amesema Mashindano hayo yatafunguliwa rasmi Agosti 16, 2026, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kabla ya kufungwa Agosti 22 na wageni kuondoka Agosti 23, 2026.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Adam Malima ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo, kuwapokea wageni kwa ukarimu na kuitumia FEASSA 2026 kuitangaza Morogoro na Tanzania.


No comments:
Post a Comment