
Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Mhe. Omari Issa atunuku shahada za umahiri na uzamivu kwa wahitimi 138 katika Mahafali ya 12 ya Taasisi ya Nelson Mandela yaliyofanyika Leo tarehe 20 Agosti 2026, NM-AIST Tengeru Arusha.
Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Balozi Maimuna Tarishi, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha tafiti, teknolojia na ubunifu unaozalishwa na Taasisi unatafsiriwa kuwa bidhaa, huduma na suluhisho halisi kwa changamoto za jamii, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.
Akizungumza katika Mahafali ya 12 ya Taasisi (NM-AIST), Balozi Tarishi amesema ubunifu haupaswi kuishia kwenye makaratasi au usajili wa hati miliki, bali unapaswa kutumika kutatua changamoto katika sekta za kilimo, ufugaji, biashara, mazingira na uchumi.
“Ubunifu usiishie kwenye makaratasi wala usajili BRELA; twende tukautafsiri kwa vitendo ili kujibu changamoto mbalimbali za jamii,” amesema Balozi Tarish.
Aidha, amewataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata NM-AIST kujitolea kuitumikia jamii ya Tanzania na Afrika, badala ya kutumia elimu kwa manufaa binafsi pekee.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Prof. Maulilio Kipanyula, amesema jumla ya wahitimu 138 wamehitimu katika mahafali hayo, wakiwa wamezalisha machapisho 219 ya kisayansi na hati miliki saba.
Amesema NM-AIST itaendelea kuhamasisha wanafunzi na watafiti kuzalisha bidhaa, kufanya ugunduzi na kuchapisha tafiti katika majarida ya kimataifa.
Pia, Profesa Maulilio Kipanyula amesema watafiti 19 wa NM-AIST wametambuliwa katika tuzo za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zinazohusisha machapisho katika majarida ya kisayansi yenye hadhi ya juu duniani.
NM-AIST inaendelea kubadili maarifa kuwa ubunifu, ubunifu kuwa bidhaa na huduma, na tafiti kuwa suluhisho la changamoto za jamii sambamba na utekelezaji wa Dira 2050.

No comments:
Post a Comment