Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Makamu wa Rais Mhe. Deogratius Ndejembi, kuitumikia nchi kwa utii, uaminifu, uzalendo, utu, busara, hekima na maarifa, huku akitanguliza maslahi ya Taifa.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 29, 2026, katika hafla ya uapisho wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Amesema nafasi ya Makamu wa Rais ni dhamana aliyopewa na Watanzania, hivyo Ndejembi anapaswa kuitumia kwa kuwatumikia wananchi wote bila kujali tofauti zao, huku akihakikisha majukumu anayokabidhiwa yanatekelezwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Aidha, Rais Samia amesema hakuna shule inayofundisha namna ya kuwa Makamu wa Rais, hivyo bidii, nidhamu, weledi na utayari wa kujifunza ni muhimu katika kumsaidia Ndejembi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Amesema kujifunza katika nafasi hiyo kunahusisha kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali, pamoja na kujifunza kutoka kwa viongozi na watendaji wengine anaofanya nao kazi.
Rais Samia amesisitiza kuwa cheo cha Makamu wa Rais si ufalme, bali ni dhamana ya kulitumikia Taifa, hivyo anayeshikilia nafasi hiyo anatakiwa kutambua wajibu huo na kuendelea kuitumikia Tanzania kwa uaminifu, uwajibikaji na uzalendo.
Aidha, amesema utekelezaji wa majukumu ya Serikali unahitaji umoja, mshikamano, ushirikiano, utulivu na uongozi bora ili kufikia matamanio na matarajio ya Watanzania.
Rais Samia amemtaka Ndejembi kutumia nafasi hiyo kwa hekima na busara, akizingatia kuwa dhamana aliyopewa ni ya Watanzania wote na kwamba maslahi ya Taifa yanapaswa kuwa msingi wa kila uamuzi na utekelezaji wa majukumu yake.





No comments:
Post a Comment