Na Shua Ndereka, OKULY BLOG, Morogoro
Serikali imewataka wananchi kuendeleza utamaduni wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kuepuka ukataji wa miti, huku akizipongeza taasisi binafsi zinazojikita katika utunzaji wa mazingira.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula Agosti 02, 2026 mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya nanenane Kanda ya Mashariki, yanayofanyika mkoani Morogoro, likiwemo Banda la Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA).
Luswetula alipata fursa ya kujionea bidhaa zinazozalishwa na wakulima wadogo kupitia kilimo ikolojia.
"Nimefarijika sana kufika katika maonesho haya ya Nanenane, tumeona mambo mengi yenye tija kubwa kwa uchumi wetu wa Tanzania. Kiuhalisia, tumeangalia namna ya utunzaji wa mazingira ambapo taasisi zetu za serikali na binafsi zimejitolea kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa bora... Tumeondokana na mbinu zilizokuwa zikisababisha uharibifu wa mazingira, ikiwemo ukataji wa miti, na sasa hali hiyo inapungua kutokana na matumizi ya teknolojia mbalimbali za uhifadhi wa mazingira," amesema Luswetula.
Kauli ya Naibu Waziri inaakisi juhudi za MVIWATA za kuhamasisha wakulima nchini kuendeleza kilimo ikolojia, ambacho ni rafiki kwa mazingira na kinachochangia uhifadhi wa maliasili pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia umuhimu wa kilimo hicho, Mratibu wa MVIWATA, Adauth Thasian, amesema wakulima wanahimizwa kutumia mbinu zinazohifadhi rutuba ya udongo, kupunguza matumizi ya kemikali, kulinda vyanzo vya maji na kupunguza ukataji wa miti, hatua ambazo pia huchangia kuzalisha chakula salama kwa walaji.
Thasian amesema, kupitia kilimo hicho, wakulima huzalisha mazao kwa kutumia mbinu zinazohifadhi mazingira, kupunguza ukataji wa miti na kulinda afya ya mlaji ikiwa mikakati ya taasisi hiyo ni kuhakikisha wakulima wadogo wanazalisha kwa njia zinazohifadhi mazingira, na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadailiko ya tabianchi.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoshirikisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga yanafanyika chini ya kaulimbiu ya mwaka 2026 isemayo, ‘Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050’ yenye lengo la kuhamasisha uzalishaji unaozingatia mahitaji ya soko na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.








No comments:
Post a Comment