
Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (MB), akimueleza Meneja wa Mikopo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Amani Shabani (kushoto), kuhusu umuhimu wa Benki hiyo kuendelea kuinua wakulima nchini, wakati alipotembelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecelaa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanayofanyika katika viwanja hivyo, Nzuguni jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, ambaye alimuongoza Mhe. Balozi Omar kutembelea Maonesho hayo yenye kauli mbiu ya ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (MB), na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, wakimsikiliza Meneja wa Mikopo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Amani Shabani, akifafanua kuhusu jitihada za benki hiyo katika kuinua wakulima nchini kupitia utoaji wa mikopo, wakati alipotembelea katika Viwanja vya Dk. John Samwel Malecelaa kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali za kilimo, mifugo na uvuvi, zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026, yanayofanyika katika viwanja hivyo Nzuguni jijini Dodoma. Maonesho hayo yana kauli mbiu ya ‘‘Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050’’.
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imezitaka taasisi za kifedha na mabenki kuongeza ushirikiano katika kufadhili sekta ya kilimo ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao, kukuza viwanda vinavyotegemea malighafi za ndani na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipotembelea Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Balozi Omar alisema umefika wakati wa kubadili mtazamo wa kuyachukulia mazao kama bidhaa za biashara pekee na badala yake kuyaona kama chanzo muhimu cha malighafi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na uchumi wa taifa.
Alibainisha kuwa uwekezaji katika uchakataji wa mazao utaongeza thamani ya bidhaa, kufungua masoko mapya, kuongeza ajira na kuwaongezea wakulima kipato kupitia mazao wanayozalisha.
Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Subira Kaswaga, alisema mamlaka hiyo imefanikiwa kutengeneza mifumo maalumu ya kidijitali inayosaidia kupambana na wizi wa fedha za wakulima ndani ya vyama vya ushirika.
Alisema mifumo hiyo imeongeza uwazi katika usimamizi wa mauzo ya mazao kwa kuwawezesha wakulima kufuatilia mazao yao, mauzo na malipo wanayostahili, hatua inayojenga imani na kuongeza uwajibikaji katika vyama vya ushirika.

No comments:
Post a Comment