
Na Erick Nenda – Dodoma
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imesisitiza umuhimu wa wananchi, hususan vijana wanaojishughulisha na kilimo, mifugo na uvuvi, kuendelea kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU), ikieleza kuwa afya ya nguvu kazi ni msingi wa uzalishaji na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Agosti 7, 2026, katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho vya Nzuguni, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Adam Mrisho, amesema afya ni msingi wa maendeleo ya taifa na vijana wanapaswa kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Dkt. Mrisho amesema kwa miaka mingi Tanzania imeendelea kunufaika na ufadhili kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo Global Fund na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), ambao umewezesha utoaji wa huduma za upimaji, elimu, dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs) pamoja na huduma nyingine muhimu.
Amesema maambukizi ya VVU yanaendelea kuwa na athari katika kipato cha familia na maendeleo ya taifa kwa ujumla, hali inayolifanya Serikali kuendelea kuwekeza katika kinga, elimu na matibabu ili kulinda ustawi wa wananchi.
Akizungumzia mabadiliko katika ufadhili wa huduma za UKIMWI, Dkt. Mrisho amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kuongeza rasilimali za ndani ili kuhakikisha huduma hizo zinaendelea kupatikana na kuimarika.
“Kuanzia mwaka 2004, wakati huduma hizi zilipoanza kutolewa na Serikali katika vituo vya afya, ufadhili wa wadau ulikuwa ukipatikana. Hata hivyo, dalili za kupungua kwa ufadhili huo zimeanza kujitokeza tangu mwaka 2012. Serikali imejipanga kuanzisha mfuko wa udhamini kwa lengo la kutokomeza UKIMWI,” amesema Dkt. Mrisho.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuchangia katika mfuko huo huku ikishirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau wengine kuhakikisha huduma muhimu za kinga, upimaji, elimu na dawa za ARVs zinaendelea kupatikana kwa wananchi bila usumbufu.
Amesema TACAIDS inaendelea kuratibu mwitikio wa taifa dhidi ya UKIMWI kwa kushirikiana na Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo, sambamba na kuweka mikakati ya kuongeza rasilimali za ndani ili kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje.
Hata hivyo, amesema ushiriki wa TACAIDS katika Maonesho ya Nanenane umeendelea kutoa fursa ya kuwafikia wananchi wengi na kuwapatia elimu kuhusu kinga dhidi ya VVU, upimaji wa hiari pamoja na matumizi sahihi ya huduma zinazotolewa na Serikali.
Dkt. Mrisho amesema makundi yanayojishughulisha na kilimo, mifugo na uvuvi yanapaswa kuendelea kufikiwa na elimu na huduma za kinga dhidi ya VVU, kwa kuwa ni sehemu muhimu ya nguvu kazi inayochochea uzalishaji na maendeleo ya uchumi wa nchi.


No comments:
Post a Comment