Tanzania ina rasilimali za maji zinazokidhi mahitaji ya nchi kwa matumizi mbalimbali, huku Serikali ikiendelea kuweka miundombinu na mikakati ya kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila mwananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema hayo Agosti 26, 2026, katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na Azam TV, akieleza kuwa Tanzania ina mita za ujazo bilioni 106 za rasilimali za maji, ikilinganishwa na mahitaji ya takribani mita za ujazo bilioni 67.
Amesema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji nchini imeendelea kuimarika, ambapo huduma hiyo imefikia asilimia 92.5 mijini na asilimia 85.2 vijijini.
Kwa mujibu wa Mhandisi Waziri, kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini, vijiji 10,758 vimefikiwa na huduma ya maji, huku vijiji 1,575 vikiwa bado havijafikiwa.
Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha vijiji vyote ambavyo bado havijafikiwa vinaunganishwa na huduma ya maji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Akizungumzia changamoto ya upotevu wa maji, Mhandisi Waziri amesema kiwango cha upotevu wa maji nchini (NRW) kwa wastani ni asilimia 40.
Ameeleza kuwa upotevu huo unatokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uvujaji wa mabomba, uchakavu wa miundombinu, hitilafu za dira pamoja na maunganisho mapya yasiyo halali.
Amesema Wizara ya Maji imeweka mkazo katika kuwawezesha wataalamu kutumia teknolojia za kisasa katika kubaini na kudhibiti upotevu wa maji, sambamba na kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
Aidha, amesema mfumo wa kubaini maeneo yenye upotevu wa maji umeanza kutumika katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Dar es Salaam na Dodoma, hatua inayolenga kurahisisha utambuzi wa maeneo yenye upotevu mkubwa na kuchukua hatua za haraka za kuudhibiti.
Mhandisi Waziri amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu, teknolojia na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha rasilimali za maji zilizopo nchini zinatumika kwa ufanisi na huduma ya maji inawafikia wananchi wengi zaidi.


No comments:
Post a Comment