
Na Beatus Maganja, Zanzibar
TANZANIA imeandika historia mpya katika ramani ya utalii barani Afrika baada ya Hifadhi ya Selous na Hifadhi ya Mpanga-Kipengere, zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kuibuka washindi katika tuzo za World Travel Awards 2026, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mamlaka hiyo kuingiza maeneo yake katika mashindano hayo makubwa ya utalii.
Ushindi huo wa kihistoria ulitangazwa wakati wa hafla ya 33 ya World Travel Awards iliyofanyika Agosti 28, 2026 katika Hoteli ya Diamonds Bijoux, Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar na kuifanya TAWA kuanza safari yake katika tuzo hizo kwa mafanikio makubwa baada ya kuingiza maeneo matatu katika kategori mbalimbali na mawili kati yake kuibuka washindi.
Maeneo hayo ni Hifadhi ya Selous, Hifadhi ya Mpanga-Kipengere pamoja na Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ambayo yaliingia katika ushindani dhidi ya baadhi ya vivutio vinavyotambulika zaidi katika sekta ya utalii barani Afrika.
Katika kategori ya Africa’s Leading Tourist Attraction 2026, Selous, Mpanga-Kipengere na Kilwa Kisiwani zilichuana na baadhi ya vivutio maarufu zaidi barani Afrika vikiwemo Pyramids of Giza nchini Misri, Table Mountain, Robben Island na V&A Waterfront nchini Afrika Kusini, Okavango Delta nchini Botswana na Lake Malawi.
Kutoka Tanzania, ushindani huo ulihusisha pia Mount Kilimanjaro, Ngorongoro Conservation Area, Amani Nature Forest Reserve na Pugu Hills Forest Reserve. Katika ushindani huo mkubwa, Hifadhi ya Selous iliibuka mshindi, ikiweka historia kwa TAWA katika ushiriki wake wa kwanza kwenye tuzo hizo.
Kwa upande wake, Hifadhi ya Mpanga-Kipengere nayo iliandika historia baada ya kuibuka mshindi katika kategori ya Africa’s Leading Honeymoon Destination 2026 ikichuana na Marrakech nchini Morocco, Mozambican Islands, Okavango Delta nchini Botswana, Red Sea Riviera nchini Misri, Volcanoes National Park nchini Rwanda pamoja na Kitulo National Park ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko, aliwashukuru Watanzania kwa kuvipigia kura vivutio hivyo na kuchangia ushindi huo huku akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ubunifu, bidii na kujituma kwa Bodi, Menejimenti na watumishi wa TAWA katika kuhakikisha maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka yanaendelea kuboreshwa na kuwa na mvuto zaidi kwa shughuli za utalii.
“Siri kubwa ya ushindi huu ni ubunifu wa vijana wangu wote, kuanzia Bodi mpaka wafanyakazi wote kujituma. Lakini kubwa zaidi ni bidii wanayoifanya katika kuhakikisha kwamba maeneo yetu yanakuwa mazuri kwa ajili ya utalii,” alisema Semfuko.
Semfuko alisema ushindi huo unaongeza nguvu katika dhamira ya TAWA ya kuendeleza utalii wa ndani na kufungua zaidi maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka kwa Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi.
“Tulimuahidi Mheshimiwa Rais kwamba TAWA tutakuwa vinara wa utalii wa ndani. TAWA tunataka kufanya makubwa Zanzibar... mtaona kishindo cha mwaka kesho,” alisema.
Naye Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange, mbali na kuwapongeza Watanzania waliovipigia kura vivutio hivyo, alisema Selous na Mpanga-Kipengere ni sehemu tu ya hazina kubwa ya vivutio vinavyosimamiwa na Mamlaka katika maeneo mbalimbali nchini.
Kabange alisema TAWA inaendelea kuboresha miundombinu katika maeneo yake ili kuongeza mvuto, kuwezesha wageni kuyafikia kwa urahisi zaidi na kuendelea kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa watalii.
“Tuna maeneo mengi zaidi. Tunaendelea kuboresha miundombinu yake ili yaweze kuvutia wageni zaidi. Tunawaahidi Watanzania kwamba tutaendelea kutoa huduma bora zaidi katika maeneo yetu,” alisema Kabange.
Ushindi wa Selous na Mpanga-Kipengere unaifanya Agosti 28, 2026 kuwa siku muhimu katika historia ya TAWA, huku ukidhihirisha uwezo wa maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka kushindana na vivutio vyenye majina makubwa katika soko la utalii la Afrika na kimataifa.
Zaidi ya kupata tuzo kwa maeneo hayo mawili, mafanikio hayo ni ushindi kwa Tanzania, kwani yanaongeza mwonekano wa hazina ya vivutio vya Taifa na kufungua fursa zaidi za kuitangaza Tanzania katika masoko ya utalii ya kikanda na kimataifa.
Ushindi huo pia unaonesha utofauti wa bidhaa za utalii zinazopatikana katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA, kuanzia wanyamapori na mandhari ya asili, maporomoko ya maji hadi urithi wa kihistoria na kiutamaduni, huku ukifungua ukurasa mpya katika juhudi za Mamlaka za kuendeleza na kutangaza vivutio hivyo.
Hii ni historia kwa TAWA, ni fahari kwa Tanzania na ni mwaliko mwingine kwa dunia kuja kuigundua Tanzania.






No comments:
Post a Comment