VIUATILIFU 132 VYAKATALIWA NCHINI, TPHPA YAZIDISHA VIFAA KUDHIBITI VISUMBUFU NA KUOKOA MAZAO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 27, 2026

VIUATILIFU 132 VYAKATALIWA NCHINI, TPHPA YAZIDISHA VIFAA KUDHIBITI VISUMBUFU NA KUOKOA MAZAO


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) , Prof. Joseph Ndunguru,akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma, leo Agosti 27, 2026, wakati akielezea mafanikio ya mwaka wa fedha 2025/2026 na Mwelekeo wa mwaka wa fedha 2026 /2027 wa Mamlaka hiyo.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA


Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imezuia na kurejesha shehena za viuatilifu visivyokidhi viwango baada ya kubaini kuwa sampuli 132, sawa na asilimia nne ya sampuli 3,463 zilizochukuliwa na kufanyiwa uchambuzi wa kimaabara, hazikukidhi viwango vilivyowekwa.

Hatua hiyo imekuja sambamba na Mamlaka kuongeza uwezo wa kudhibiti visumbufu vya mimea nchini kwa kuagiza ndege nyuki nyingine 20, huku ikiwa tayari ina ndege nyuki 21 zinazotumika katika kudhibiti wadudu na ndege waharibifu wa mazao.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma, leo Agosti 27, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema hatua za udhibiti wa viuatilifu zinalenga kuhakikisha wakulima wanapata bidhaa salama, zenye ubora na zilizosajiliwa.

Amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, TPHPA ilikagua maduka 5,157 ya viuatilifu, ilitoa vibali 3,831 vya kuingiza viuatilifu nchini na kusajili viuatilifu vipya 508.

“Katika uchambuzi huo, sampuli 132, sawa na asilimia nne, hazikukidhi viwango na wahusika waliagizwa kurejesha shehena hizo,” amesema Prof. Ndunguru.

Aidha, amesema Januari 2026 Mamlaka iliondoa sokoni viuatilifu 205 vilivyobainika kuwa na viambata amilifu hatarishi baada ya kufanyiwa tathmini ya kiafya na kimazingira, huku viuatilifu 675 vikiondolewa kwenye orodha ya vilivyosajiliwa kutokana na kutohuishwa kwa usajili wake kwa zaidi ya miaka 10.

Katika kuimarisha udhibiti wa visumbufu vya mimea, Prof. Ndunguru amesema TPHPA inaendelea kuongeza vitendea kazi, ikiwemo ndege nyuki 20 ambazo zimeagizwa ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na milipuko ya wadudu na ndege waharibifu wa mazao.

Taarifa ya TPHPA inaonesha kuwa Mamlaka tayari imenunua ndege maalumu aina ya Thrush 510P2+ yenye uwezo wa kubeba hadi lita 1,930 za kiuatilifu na kunyunyizia eneo kubwa kwa wakati mmoja.

Hatua hizo zinaimarisha uwezo wa Serikali kulinda mazao dhidi ya visumbufu na kupunguza hasara kwa wakulima. Katika mwaka wa fedha 2025/2026, TPHPA ilidhibiti kwelea kwelea milioni 233.5 waliovamia wilaya 21 kwa kutumia ndege na ndege nyuki, na kuokoa takribani tani 1,092,780 za mazao ya nafaka ambazo zingeweza kupotea.

TPHPA imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha ukaguzi katika vituo vya mipakani, kudhibiti viuatilifu bandia na visivyosajiliwa, pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kutambua na kudhibiti visumbufu vya mimea.

Mamlaka pia inalenga kuimarisha mfumo wa tahadhari wa mapema (Early Warning System) ili kutambua viashiria vya milipuko ya visumbufu na magonjwa ya mimea mapema, kuchukua hatua kwa wakati na hivyo kuokoa mazao.

No comments:

Post a Comment