Na Okuly Julius, OKULY BLOG ,DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza fursa mpya ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 10 wa Kitanzania kwenda kusoma nchini Urusi, kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Agosti 13,2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa wanafunzi hao wamepata fursa hiyo kutoka Chuo Kikuu cha RUDN kilichopo Moscow, kufuatia ziara rasmi ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi iliyofanyika Juni mwaka huu.
Amesema wanafunzi hao wanatarajiwa kuondoka nchini Septemba Mosi mwaka huu kuelekea Moscow, ambako wataanza kambi maalumu ya mafunzo (bootcamp) ya maandalizi itakayodumu kwa takribani miezi 10 kabla ya kuanza masomo yao ya shahada ya kwanza.
“Katika kipindi cha bootcamp, Serikali ya Urusi itagharamia asilimia 80 ya gharama na Samia Scholarship Extended itagharamia asilimia 20,” amesema Profesa Mkenda.
Ameongeza kuwa baada ya wanafunzi hao kumaliza kambi hiyo na kuanza masomo rasmi ya shahada, Serikali ya Urusi itagharamia asilimia 100 ya masomo yao.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, wanafunzi hao 10 wanaungana na wanafunzi wengine 50 waliotangazwa awali, hivyo kufanya jumla ya wanafunzi watakaonufaika na mpango huo kufikia 60.
Amesema wanafunzi hao watasomea fani za Data Science, Artificial Intelligence (Akili Unde) na Allied Sciences, ambazo ni miongoni mwa maeneo muhimu katika kukabiliana na mahitaji ya ujuzi wa kisasa.
Profesa Mkenda amesema wanafunzi 50 waliopata fursa awali wataanza kambi yao ya mafunzo katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela (NM-AIST), Arusha, kuanzia Septemba 14 mwaka huu, huku wakitakiwa kuripoti chuoni hapo Septemba 13.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi, Profesa Mkenda alisema wanafunzi hao walichaguliwa kwa kuzingatia ufaulu wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita, hususan katika michepuo ya sayansi ya PCM, PGM na PMC.
Amesema wanafunzi 50 waliokuwa katika nafasi za kwanza hadi 50 walichaguliwa kwenda Arusha, huku waliokuwa nafasi ya 51 hadi 60 wakipata fursa ya kwenda kusoma nchini Urusi.
“Kati ya wanafunzi 10 wanaokwenda Urusi, wanafunzi nane wanatoka katika shule za Serikali na wawili wanatoka shule binafsi,” amesema.
Profesa Mkenda amesisitiza kuwa Serikali imezingatia uwazi na uadilifu katika mchakato wa uteuzi ili kuhakikisha fursa hizo zinatolewa kwa wanafunzi wenye uwezo unaostahili.
Aidha, Waziri huyo amesema Wizara inaendelea kuratibu maandalizi ya safari, ikiwamo kuwapatia pasipoti wanafunzi tisa ambao hawakuwa nazo, ili kuwawezesha kuondoka nchini kwa wakati.
Amesema majina ya wanafunzi wote 10 waliochaguliwa yatawekwa kwenye tovuti rasmi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya taarifa zaidi kwa umma.





No comments:
Post a Comment